UFINYU WA BAJETI SEKTA YA MICHEZO TATIZO SONGEA. - Rhevan Media

UFINYU WA BAJETI SEKTA YA MICHEZO TATIZO SONGEA.




WB
Na Mwandishi Maalum – Songea
Ufinyu wa Bajeti katika sekta ya michezo umechangia kwa kiasi kikubwa kwa kituo cha Michezo cha kanda ya Kusini- Songea kushindwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa makocha, marefarii, madaktari wa michezo, uongozi na utawala katika michezo.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa kituo hicho Eliufoo Nyambi wakati akisoma taarifa ya kituo kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura wakati alipotembelea kituo hicho ili kuona shughuli za michezo wanazozifanya.
Nyambi alisema miaka ya nyuma kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi ya aina tofauti ya michezo na kufanikiwa kupata wataalamu wa ngazi za makocha, marefa, madaktari wa michezo, utawala na uongozi wanaotoa mafunzo na huduma za kimichezo kutoka mikoa 13 na wengine kupata sifa za kujiunga na chuo cha Maendeleo ya michezo kilichopo Malya wilayani Kwimba.
“Kuanzia mwaka 2011 hadi sasa kituo hiki hakijatoa mafunzo ya michezo katika mikoa inayoihudumia ya kanda ya Kusini ikiwa ni pamoja na upimaji wa viwanja hii ni kutokana na ufinyu wa bajeti uliopo”, alisema Nyambi.
Kwa upande wake Mhe. Naibu Waziri Wambura alisema nia ya Serikali ni kuimarisha michezo ili watu wapate muda wa kucheza kwani michezo ni afya, chanzo cha ajira, kujenga mahusiano mazuri katika jamii na Serikali kupata chanzo cha kukusanya maduhuli.
Mhe. Wambura alisema Serikali itaangalia namna ya kukiwezesha na kukiboresha kituo hicho ili kiendelee kutoa mafunzo hayo ambayo yakifanyika yatasaidia kupunguza gharama kwakuwa yanawakusanya wanamichezo wengi katika eneo moja na walimu wa michezo wanaenda kutoa mafunzo.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Benson Mpesya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Songea alisema hivi sasa mafunzo ya michezo yanatolewa na Asasi binafsi lakini kama Kituo hicho kitatoa mafunzo itawasaidia washiriki kupata elimu ya michezo na vyeti vya ushiriki vinavyotolewa na Serikali.
Mwaka 1980 Serikali ilianzisha vituo vya michezo viwili ambavyo ni kituo cha michezo cha Kanda ya Kaskazini kilichopo mkoani Arusha na Songea.
Kituo cha Michezo Songea kinahudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Iringa , Mbeya, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Dodoma na Songwe.




Previous
Next Post »