TAKUKURU YABAINI WAFANYAKAZI WENGINE 5 HEWA KATIKA JIJI LA MWANZA. - Rhevan Media

TAKUKURU YABAINI WAFANYAKAZI WENGINE 5 HEWA KATIKA JIJI LA MWANZA.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU ) Mkoani Mwanza imebaini kuwepo kwa watumishi wengine hewa watano katika halmashauri ya jiji la mwanza ambao wanadaiwa kutumia nyaraka za kughushi kukopa fedha katika mabenki mbalimbali, huku baadhi ya halmashauri mkoani humo zikidaiwa kuwasilisha orodha pungufu ya wafanyakazi hewa tofauti na orodha ya watumishi hewa 334 iliyowasilishwa kwa mkuu wa mkoa huo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale amesema hali hiyo imesababishwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu wa halmashauri ya jiji la Mwanza kutoa taarifa za udanganyifu kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, ambapo taasisi hiyo imeahidi kuzifanyia uchunguzi wa kina tuhuma za watumishi hewa kabla ya kuwachukulia hatua stahiki.
 
Aidha, mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza ameongeza kuwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, TAKUKURU mwanza imeokoa fedha za umma zaidi ya shilingi milioni 90, ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara katika halmashauri ya wilaya ya Magu, pesa hiyo ilikuwa imegawiwa kwa mtumishi mmoja wa idara ya ujenzi kama masurufu maalum, huku kazi ya ukarabati wa barabara hiyo ikiwa haujafanyika.
 
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita mwaka huu, imewafikisha mahakamani watuhumiwa 10, akiwemo aliyekuwa Meya wa manispaa ya Ilemela Henry Matata pamoja na Mhandisi wa manispaa hiyo Justin Lukaza kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kutokana na kukiuka sheria ya manunuzi ya umma kwa kutoa zabuni ya kutoza ushuru katika stendi ya mabasi ya Buzuruga kinyume cha utaratibu.
Previous
Next Post »