RC MWANZA ATUMBUA WATANO ILEMELA. - Rhevan Media

RC MWANZA ATUMBUA WATANO ILEMELA.




Mkuu wa wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella
Mkuu wa wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella 
By Ngollo John, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Mwanza. Mkuu wa wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewasimamisha kazi maofisa watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka.
Akiwa katika ziara ya siku moja ya kujitambulisha wilayani Ilemela leo, Mongella ameagiza kushushwa cheo kwa ofisa wa ardhi wa wilaya hiyo, Anicet Rweyemamu kwa tuhuma za kushindwa kusimamia watumishi walio chini yake wanaotuhumiwa kupokea Sh12 milioni kutoka kwa mwananchi mmoja aliyekuwa akitaka ardhi, lakini hajapewa hati hadi sasa.
Wengine walioangukiwa na rungu la mkuu huyo ni Debora Tongora ambaye pamoja na Alex Chigulu wanatuhumiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kuwapatia viwanja.
Wakati Tongola tayari amefunguliwa mashtaka dhidi ya tuhuma hizo, Chigulu amehamishiwa mkoani Singida lakini Mongella ameagiza arejeshwe Mwanza ili afikishwe mahakamani.
“RPC wasiliana na mwenzako wa Singida ili huyo mtumishi atiwe mbaroni muda huu na kesho arejeshwe Mwanza kukabiliana na mashtaka dhidi yake. Hatuwezi kuwavumilia watumishi wanaoharibu sehemu moja halafu wanakimbia uhamisho kwenye maeneo mengine,” amesema Mongella
Ofisa uvuvi wa Kituo cha Kirumba, Ivon Maha ameshushwa cheo huku Peter Revelian akiondolewa kutoka nafasi ya mweka hazina.
Watumishi hao wa Idara ya Uvuvi wameondolewa madarakani baada ya kutuhumiwa kuhusika na upotevu wa zaidi Sh40 milioni zilizotokana na kodi na ushuru.
Awali, Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Manju Msambya alimweleza Mongella kuwa wilaya hiyo tayari imetengeza madawati 7, 200 kati ya 29, 000 yanayohitajika.
“Wilaya yetu inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu katika shule za umma na tayari tumewasilisha maombi ya walimu wapya,” amesema Msambya
Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulungi alimuahidi mkuu huyo wa mkoa kuwa baraza lake litaongeza juhudi katika usimamizi wa utendaji kwa watumishi wa halmashauri hiyo.


Previous
Next Post »