RC MULONGO AMTUMBUA JIPU OFISA MTENDAJI ALIYESABABISHA MAUAJI. - Rhevan Media

RC MULONGO AMTUMBUA JIPU OFISA MTENDAJI ALIYESABABISHA MAUAJI.

MKUU wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo, amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Rorya kukatisha mkataba wa ajira wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kenyamasoma, baada ya kushindwa kuwajibika katika tukio la mauaji lililosababisha vifo vya wanawake wawili wiki iliyopita.

Mulongo pia amemwagiza mkurugenzi kwa kushirikiana na baraza la madiwani, kuitisha uchaguzi mdogo wa mwenyekiti mpya wa kijiji hicho, baada ya mwenyekiti wa sasa naye kushindwa kutimiza wajibu wake kikatiba na kuruhusu mauaji ya watu wasio na hatia kufanyika bila kuchukuliwa kwa hatua zozote.
Alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kenyamosoma, alipokwenda baada ya kutokea mauaji ya wanawake wawili waliouawa kwa tuhuma za ushirikina.
Mulongo alisema isingewezekana maandalizi ya mauaji ya vikongwe hao yafanyike ndani ya kijiji huku viongozi wakishindwa kuchukua hatua zozote za kuzuia bila kuziarifu mamlaka husika, vikiwamo vyombo vya dola.
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa taarifa za mauaji hayo zilivifikia vyombo vya dola zaidi ya saa tano, baada ya tukio hilo la kinyama kufanyika huku viongozi wa kijiji wakiwa kimya bila kuziarifu mamlaka husika, jambo linaloashiria kuwa walikula njama na wahusika waliotekeleza mauaji hayo.
Butiku Warioba, mtoto wa mmoja wa wanawake waliouawa, Nyakorema Warioba, alisema Aprili 11, mwaka huu, saa 3.30 asubuhi, mama yake aliuwawa na kundi kubwa la wananchi wakiwa vijana kwa kumtuhumu kuwa mchawi na ameshirikiana na mama yake wa kambo kumuua kaka yake na Butiku.
Warioba alisema kabla ya tukio, babu yake aitwaye NyamuhangaWarioba, alipiga ngoma ya kuwaalika wananchi kuashiria kulikuwa na jambo la dharura, akiwataka wanakijiji wote kuhudhuria na kwamba yeyote ambaye angeshindwa kuhudhuria angetozwa faini ya sh. 20,000.
Alisema wakati wakienda kwenye mkutano huo, walikutana na kundi hilo na kuanza kumshambulia mama yake kwa kumpiga na kumrejesha nyumbani kwake. Walipofika, walimwingiza ndani ya nyumba kisha kuichoma kwa moto na kusababisha kifo.
Mwingine aliyekumbwa na masahibu hayo ni Ghati Ndege, ambaye aliuawa kwa stahili hiyo hiyo ya kuchomewa ndani ya nyumba saa tano asubuhi, saa moja na nusu baada ya kuuawa Nyakorema.
Previous
Next Post »