NAIBU WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATEMBELEA KAMBI YA MAAFA ZANZIBAR. - Rhevan Media

NAIBU WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATEMBELEA KAMBI YA MAAFA ZANZIBAR.



 Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman akisalimiana na wawakilishi wa mashirika ya WHO na UNICEF alipowasili katika kambi ya maafa kuona mazingira ya Kambi hiyo iliyopo Skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe C nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman akizungumza na baadhi ya wananchi waliohifadhi katika kambi ya maafa Mwanakwerekwe C.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.


Na Ramadhan Ali-Maelezo Zanzibar.
MAAFISA wanaoshughulikia wananchi waliohifadhiwa katika kambi ya maafa Mwanakwerekwe C wameshauriwa kutoa elimu ya Afya kwa wananchi hao ili kuwaepusha na maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Naibu Waziri wa Afya Bi. Harusi Said Suleiman ametoa ushauri huo alipoitembelea kambi ya maafa kuona mazingira  na matatizo yanayowakabili katika kambi hiyo akiambatana na wawakilishi wa Mashirika ya WHO na UNICEF waliopo Zanzibar.

Amesema  kambi inakusanya watu wengi wenye desturi na taratibu za maisha tofauti hivyo suala la kutoa elimu ya Afya itakayosaidia maambukizi ya maradhi ni kitu muhimu .
Amewata wananchi hao  kufuata taratibu na maelekezo ya maafisa wa kambi hiyo ikiwemo  kunywa maji yaliyotiwa dawa na kukosha mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula ili wawe walimu wazuri watakaporejea kwenye makaazi yao.

Afisa Msaidizi wa Kambi ya maafa Makame Khatib Makame amemueleza Naibu Waziri wa Afya kwamba hivi sasa kambi inawatu 420 wakiwemo wanawake 240.

Amesema huduma zote muhimu zinatolewa ndani ya kambi hiyo na wameanzisha utaratibu wa kuwapeleka  na kuwarejesha watoto wanaosomo katika skuli zao.

Wananchi wanaohifadhiwa katika kambi ya maafa wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwasaidia watakaporejea katika makaazi yao kwa vile wamepoteza vifaa vingi vya matumizi baada ya nyumba zao kujaa maji. 


Previous
Next Post »