Mwendesha Mashtaka, Wakili wa serikali, Michael Ng’hoboko alidai kwamba kati ya Aprili 29, mwaka 2013 na Machi, 27, mwaka 2014 mshitakiwa kwa makusudi alilipa mishahara ya wafanyakazi hewa ya zaidi ya Sh. milioni 29.4 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, Ng’hoboko alidai kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staafu kazi kwa kipindi cha muda mrefu, kupitia akaunti yake iliyopo katika Benki ya NMB, Tawi la Singida.
Mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo yote 57 na hivyo kesi yake imeahirishwa hadi Aprili 27, mwaka huu itakapotajwa tena.
Hakimu Minde alisema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na kwamba atapaswa kutoa fedha taslimu Sh. milioni 14.7 mahakamani hapo au awe na mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.
Wiki iliyopita, serikali ilitangaza kuanza uchunguzi kuwabaini watumishi wote waliokuwa wakijilipa mishahara ya wafanyakazi hewa ili hatimaye wachukuliwe hatua.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alisema kuna mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambaye alikuwa akijilipa mishahara 17 ya wafanyakazi hewa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki, watumishi hewa wameshaisababishia serikali hasara Sh. bilioni 7.6 kuanzia Januari hadi Machi.
Chanzo cha uhakika kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kilieleza Nipashe kuwa tayari serikali imeanza uchunguzi wake kuwabaini maofisa utumishi waliokuwa wakitafuna fedha hizo ili wakamatwe.
Mtoa taarifa wetu alisema ukamataji huo utahusisha hazina, waliolipa, wafanyakazi wa wizarani na hata Halmashauri, na kwamba ni suala ambalo linahitaji upelelezi wa kitaalamu kuwabaini wahusika.
"Wale waliokuwa wakitajirika na mishahara hewa siku zao zinahesabika na uchunguzi unaofanyika si wa kawaida," kilisema chanzo chetu ambacho hakikupenda kutajwa jina.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ana kilango Malecela baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa.
Baada ya taarifa hiyo, Ikulu ilifanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza na awamu ya pili ya uchunguzi bado unaendelea.
Sign up here with your email