MAHAKAMA YATUPA SHERIA YA MATUSI KENYA. - Rhevan Media

MAHAKAMA YATUPA SHERIA YA MATUSI KENYA.

KatibaImage copyrightGetty
Image captionJaji Ngugi amesema makosa yanayoangaziwa yanaweza kushughulikiwa na sheria nyingine
Mahakama Kuu jijini Nairobi imeamua kwamba Kifungu cha Sheria ambacho kimekuwa kikitumiwa kuwafungulia mashtaka watu kuhusiana na ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii Kenya ni haramu.
Jaji wa Mumbi Ngugi alisema kifungu hicho, cha kutumia vibaya kifaa cha mawasiliano, kinakiuka katiba.
Kifungu hicho nambari 29 katika Sheria ya Habari na Mawasiliano Kenya Nambari 3 ya 1998 hupendekeza faini ya Sh50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela, au adhabu zote mbili, kwa mtu anayepatikana na hatia.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mwanasheria Mkuu walikuwa wametetea sheria hiyo wakisema ililenga kulinda sifa za wengine.
Jaji Ngugi alisema maelezo ya kifungu hicho ni mapana sana na pia baadhi ya makosa yanayolengwa kwenye kifungu hicho yameangaziwa katika sheria nyingine.
Aidha, alisema hakijatimiza matakwa ya Kipengele 24 cha Sheria ambacho kinaeleza ni katika hali gani ambapo haki za kimsingi zinaweza kubanwa. Aidha, alisema kifungu hicho kinakiuka Kipengele nambari 33 cha Katiba.
“Iwapo lengo ni kulinda sifa za watu wengine, basi hilo limeangaziwa kwenye sheria ya kuwaharibia sifa watu wengine,” Jaji Ngugi alisema kwenye uamuzi wake.

Jaji huyo alitaja mfano wa kesi tofauti dhidi ya mwanablogu mmoja ambaye aliamriwa kulipa Sh5 milioni na mahakama baada ya kushtakiwa chini ya sheria za kuwaharibia watu sifa.
Jaji Ngugi alikuwa akitoa uamuzi katika ombi la mwanablogu Geoffrey Andare aliyekamatwa Aprili 2015 na kufunguliwa mashtaka ya kutumia vibaya kifaa cha mawasiliano kutokana na ujumbe alioandika kwenye mitandao ya kijamii.
Mlalamishi alipinga mashtaka hayo akisema sheria hiyo inabana uhuru wa kujieleza mtandaoni.
Jaji alisema DPP hawezi kuendelea na kesi hiyo kwa msingi wa sheria hiyo.
Wakenya mtandaoni wamefurahia hatua hiyo ya Jaji Ngugi na tangu jana jioni jina lake limekuwa likivuma kwenye Twitter.
Kuna wanaomsifu kwa kutetea uhuru wa wananchi kujieleza lakini wengine wanahisi kwamba amekuwa akiharamisha vifungu vingi sana vya sheria.
Mfano ni Stephen Wambua anayesema uamuzi wa jaji huyo unafaa kuwekwa kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness Book of World Records.
JObiz naye anasema Jaji Ngugi alitoa uamuzi wa busara na kwamba kosa pekee linafaa kuwa kumtoa mtu uhai.
Lakini mwanahabari Oliver Mathenge ana mtazamo tofauti na kwa maoni yake Jaji Ngugi amezidi na huenda wakati mmoja akaamua kwamba Katiba yenyewe inakiuka Katiba. Anasema watu hawafai kuruhusiwa kamwe kuwatusi wengine.
Jaji Ngugi, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akihudumu katika kitengo cha Mahakama Kuu kilichoangazia masuala ya Kikatiba na Haki za Kibinadamu jijini Nairobi amehamishiwa mji wa Kericho katika eneo la kusini Magharibi mwa Kenya. Amehudumu katika kitengo hicho tangu Septemba 2014
Atakuwa jaji mwandamizi wa Mahakama Kuu mjini humo.
Tangazo la kuhamishwa kwake lilifanywa saa chache kabla yake kutoa uamuzi katika kesi hiyo ya Andare. Jaji Mkuu Willy Mutunga aliwahamisha jumla ya majaji 105 ambao wanatakiwa kuanza kazi katika vituovya vipya Juni 2.
Previous
Next Post »