ASILIMIA 30 WANA MIKATABA YA AJIRA NCHINI. - Rhevan Media

ASILIMIA 30 WANA MIKATABA YA AJIRA NCHINI.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama  
By Julius Mathias, Mwananchi jmathias@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Kati ya Watanzania milioni 24 wenye sifa za kufanyakazi nchini, mwajiriwa mmoja kati ya watatu ana mkataba wa muda mfupi ambao unaweza ukasitishwa muda wowote na kumrudisha mhanga kwenye lindi la umaskini.
Hilo limebainishwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama wakati wa mkutano wa kwanza wa Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) na wadau wa ajira nchini uliotathmini ajira zenye staha kwa vijana wa Kitanzania.
Akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya waziri huyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira kutoka wizara hiyo, Joseph Nganga amesema kuna changamoto nyingi kwenye mazingira ya kazi nchini lakini serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuzishughulikia.
“Asilimia 30 ya watumishi wanaopata mshahara wana mikataba ya muda mfupi ambayo inaweza ikavunjwa kwa taarifa au ujumbe mfupi. Watu milioni 4.3 wapo kwenye sekta isiyo rasmi. Hawa wote wanafanya kazi kwenye mazingira yasiyo na staha na muda wowote wataposimamishwa watakuwa masikini kwa kukosa kipato,” alisema Nganga.
Amefafanua kuwa zaidi ya nusu (asilimia 58.8) ya wafanyakazi wa mashambani wamo kwenye kundi lisilo na staha huku mtu mmoja kati ya 10 walioajiriwa kwenye mashirika ya umma anatumikia katika mazingira hatarishi wakiwemo asilimia 2.2 ya watumishi wa serikali.
Ameeleza kuwa kwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliopo: “Serikali imedhamiria kuimarisha viwanda na kilimo. Kwa kufanya hivyo, inataka asilimia 40 ya ajira zote itokane na viwanda. Hilo litasaidia kuboresha ajira na kuinua maisha ya vijana na Watanzania kwa ujumla.”



Wakati serikali ikitekeleza mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati, ILO imeshauri matumizi ya teknolojia kwenye sekta zinazoajiri watu wengi ili kukidhi mahitaji ya vijana wengi.
Amesema Tanzania ina watu wengi wanaofanya kazi ikilinganishwa na mataifa mengine duniani lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba ajira nyingi zilizopo hazina staha hivyo kutowavutia vijana.
“Wengi wanafanya kazi ndogo ndogo ambazo hazikidhi mahitaji yao. Vijana wengi niliozungumza nao wanataka ajira zenye fursa ya kukua kitaaluma na kujitosheleza kwa kipato. Ili kufikia adhma hiyo ni jambo jema endapo serikali itaona umuhimu wa kutumia teknolojia kwenye mkakati wake wa kukuza uchumi ndani ya miaka mitano ijayo,” amesema Mary Kawar, Mkurugenzi Mkazi wa ILO nchini.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri nchini (ATE), Joyce Nangai alisema kwa kiasi kikubwa umaskini unachangiwa na kukosekana kwa ajira pamoja na mazingira duni ya kazi zilizopo hivyo chama chake kinaangalia namna ya kuishughulikia changamoto hiyo.





Previous
Next Post »