MADEREVA KUHUDUMIWA WAKIWA BARABARANI. - Rhevan Media

MADEREVA KUHUDUMIWA WAKIWA BARABARANI.

KATIKA jitihada za kujali afya za madereva wanaosafirisha ama abiria au shehena kwa masafa marefu, wadau wa afya na usafirishaji wamefungua vituo pembeni mwa barabara ili kuwahudumia.

Kwa kuanza vimeanzishwa vituo vitatu kwenye barabara ya Dar hadi Tunduma, ambavyo madereva watapumzika na kupatiwa huduma muhimu kuanzia matibabu na ushauri bila kutozwa gharama.
Vituo vitatu vya mwanzo vimefunguliwa katika barabara kuu kuanzia Dar hadi Tunduma, wakiwa jijini Dar es Salaam kituo cha kuwahudumia kipo bandarini, kingine kimejengwa Iringa na cha tatu kinapatikana Tunduma kwa ajili ya kuhudumia wanaovuka mpaka ili kuingia ama kutoka Zambia.
Asasi ya Impala Terminals pamoja na kampuni ya nishati ya Puma Energy Foundations ndiyo wanaoendesha vituo vya afya kando kando ya barabara.
Meneja Mkuu wa Puma Energy, Philippe Corsaletti, anasema kwa kutambua na kujali umuhimu wa afya za madereva wao kumewasukuma kujihusisha na mpango huo ambao utasaidia madereva kupata matibabu katika vituo hivyo bila gharama.
Anaongeza kuwa madereva wa malori na jamii inayovizunguka vituo hivyo vya afya watapata huduma za afya bure, ikiwa ni uchunguzi wa magonjwa yakiwamo ya ngono (STI), kifua kikuu (TB), kupima malaria na ushauri kutoka kwa wataalamu wabobezi.
“Lengo la kuanzishwa kwa vituo hivyo ni kujali afya za madereva hawa kwani mara nyingi wanakabiliwa na changamoto ya kupata huduma ya afya wanapokuwa safarini.”anaongeza Corsaletti.
Anataja eneo jingine la kipaumbele kuwa ni kupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa madereva hao ambao baadhi yao hufanya ngono zisizo salama kutokana na kuwa muda mrefu barabarani pia mbali na wake zao.
Kadhalika ni kuwapatia mapumziko kwani madereva wa malori wanalazimika kuwa barabarani kipindi kirefu hivyo kuendelea kupumzika au kuchukua mapumziko ya kawaida katika vituo tofauti barabarani wanaposafiri kati ya Dar es Salaam na nchi za jirani ni lengo jingine.
Mbali na kupatiwa kwa huduma za afya pia watapewa mafunzo ya udereva wa kujihami yanayotolewa katika vituo hivyo kupitia mpango wa kufundisha madereva unaoendeshwa na North Star Alliance ikiwa ni pamoja na kudhibiti uchovu, msongo wa mawazo, milo na athari zake katika afya, udereva wa kujihami, usalama barabarani na elimu ya rika.
Corsaletti anasema moja ya shughuli zao wanazozifanya ni kusafirisha mafuta ndani na nje ya nchi na kwamba husafirisha kati ya malori 50 hadi 80 barabarani kwa kila siku, hivyo wanawajibika kuwajali madereva ambao ni msingi muhimu wa sekta hiyo.
Anasema katika kipindi cha miaka mitatu hawajapata ajali ambayo imesababisha vifo kwa kuwa madereva wao huzingatia usalama barabarani.
Anaeleza kuwa ndiyo maana wameamua kuingia katika mpango wa kuanzisha vituo vya afya pembeni ya barabara kwa kuwa wanaamini madereva wa malori ni moja ya kundi ndani ya jamii ambalo liko katika hatari kubwa kiusalama na kiafya.
Anasema kuanzishwa kwa vituo vya afya kwa madereva itawasaidia katika kujali afya zao kwani walikuwa wanapata changamoto katika kupata huduma za afya.
“Shughuli zetu zinaweza kuwa salama tu pale watu waliotuzunguka wanapokuwa salama na madereva wanachangia sehemu kubwa katika hili,” anasema Corsaletti.
Aidha anasema kampuni yake inazingatia mambo yafuatayo kila mtu anastahili kuwa na afya njema, ajali za barabarani zinazuilika, watumiaji wa barabara wanastahili kujaliwa na kila mmoja analo jukumu la kusimamia utekelezaji wa masuala hayo.
Anaeleza kuwa katika kutimiza majukumu yao wamejikita kuhakikisha kwamba watu wanaofanya kazi pamoja na jamii inayowazunguka wanakuwa salama na wenye afya bora.
“Tumejikita sana katika kuendeleza jamii na hii inakuwa ni sehemu ya maendeleo ya kudumu. Tunazingatia na kukusudia kufika viwango vya juu katika masuala ya usalama na mazingira kwa kuwekeza katika mipango ya muda mrefu ndani ya jamii yetu,” anasema Corsaletti.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kituo hicho kwa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John, alisema mashirika yaliyoshirikiana katika kutengeneza mpango huo yanastahili pongezi kwa kujali afya za madereva na jamii inayowazunguka kwenye maeneo ya kupunguza maambukizi ya magonjwa kama Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
“Tumeona miaka kadhaa kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya VVU kutokana na mazingira ya kazi zinazowazunguka madereva vituo hivi vitakuwa ni ukombozi mkubwa kwa madereva ”,anasema John.
Previous
Next Post »