MABADILIKO YA TABIA YA NCHI YASABABISHA KUKAUKA KWA MITO 40 KILOMBERO. - Rhevan Media

MABADILIKO YA TABIA YA NCHI YASABABISHA KUKAUKA KWA MITO 40 KILOMBERO.

Tatizo la mabadiliko ya Tabianchi na uharibifu wa misitu na Mazingira katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro limeababisha kukauka kwa mito zaidi ya 40 katika wilaya hiyo ambapo sasa imebaki mito 38 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo wilaya hiyo ilikuwa na mito 78 inayotirika mwaka mzima.
Afisa misitu wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro,Magai Fares amesema tatizo hilo la mabadiliko ya Tabianchi na uharibifu wa misitu pia limeathiri uzalishaji wa mazao ya Kilimo kwa baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakipata mvua zisizotabirika na kwamba baadhi ya mito iliyokuwa inatiririka Mwaka mzima zamani,sasa imebaki kuwa mito ya msimu inayokauka kabisa wakati wa kiangazi.
 
Nae diwani wa kata ya Mngeta wilayani Kilombero,Felician Kigawa amesema wananchi wengi wa wilaya ya Kilombero wanatambua tatizo la Mabadiliko ya Tabianchi kwani baadhi ya mazao yamekuwa yakikauka ingawa amesema kuimarika kwa uhifadhi wa misitu ya Kilombero na Udzungwa kumekuwa na manufaa ya upatikanaji wa mvua za kutosha kwa baadhi ya maeneo.
 
Akiongea na wananchi wa baadhi ya vijiji vya wilaya ya Kilombero vinavyotekeleza mradi wa usimamizi shirikishi wa Misitu ambao ni wa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na mtandao wa jamii wa uhifadhi wa Misitu Tanzania mjumita chini ya ufadhili wa serikali ya Norway, mratibu wa mradi huo,Elinas Monga amesema mradi huo uitwao Ecoprc unalenga kuishirikisha jamii kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kutilia mkazo uhifadhi wa misitu ya asili. 
Previous
Next Post »