Wapiganaji wa kundi la Boko Haram wameishambulia kambi ya jeshi la Nigeria mapema asubuhi ya leo na kuua idadi kubwa ya wanajeshi huko Borno.
Mwanajeshi mmoja aliyeko Borno ameielezea BBC kuwa''wapiganaji wa Boko Haram waliwavizia na kuwashambulia alfajiri na mapema wakiwa wamelala.''
''Wapiganaji hao walikuwa wamejihami kwa silaha kali na kusababisha maafa makubwa upande wa wanajeshi''
Kambi hiyo ndogo iliyoko katika kijiji cha Kareto ilikuwa na wanajeshi wachache ambao kazi yao ilikuwa ni kulinda ngome kabla ya kikosi kikubwa zaidi kuwasili.
Hata hivyo mwanajeshi huyo anasema kuwa idadi ya wapiganaji hao ilikuwa kubwa mno hata wanajeshi kadhaa walitoroka ilikuokoa maisha yao.
''Walikuwa na silaha nzito nzito na kali kuliko zetu'' afisa huyo aliiambia idhaa ya BBC Hausa.
''Tuliwapoteza wenzetu wengi,,,,,wengi sana,, sijui hata ni wangapi waliojeruhiwa''
''Baadhi yetu walitoroka maji yalipozidi unga''
''Tuligundua idadi ya wavamizi ilikuwa ni kubwa kuliko yetu'' mwanajeshi mwengine aliiambia shirika la habari la AFP.
Wapiganaji kadhaa waliuawa katika makabiliano hayo yaliyodumu kwa saa kadhaa kulingana na wenyeji wa kijiji hicho.
Hata hivyo jeshi lilijitahidi na kuikomboa kambi hiyo baada ya mashambulizi ya angani kuwasili na kuwaokoa wanajeshi walikuwa wamesakamwa ardhini.
Idadi kamili ya waliouawa haijajulikana.