Aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya nne, Stephen Wasira, amemshangaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba aliposema kuwa uwajibikaji katika utawala wa awamu ya nne ulikuwa ni wa kuleana.
Kauli ya Wasira imekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila siku kumnukuu Makamba akisema uwajibikaji katika Serikali ya awamu hiyo haukuwa wa kuridhisha kwasababu kulikuwa na utamaduni wa kuoneana haya, kujuana na kusitiriana.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi jijini Dar es Salaam jana, Wasira alieleza kushangazwa na kauli hiyo ya Makamba akisema yawezekana aliyelelewa ni yeye.
“Labda alilelewa yeye…kama rafiki yangu Makamba anasema kulikuwa na kuleana, mimi kwa upande wangu sikulelewa nilifanya kazi na nikatimiza wajibu wangu kama nilivyopewa na Rais.
“Sasa kama aliona kulikuwa kuna kuleana mimi sijui yeye ndiye anajua maana mimi sikulelewa. Kama unafanya makosa halafu unaachwa huondolewi hapo ni kuleana.
“Na yeye inawezekana alilelewa maana kuna watu wanasema kuingia kwake tano bora ya urais alipendelewa labda huko ndio kulelewa ndio maana akasema hivyo,”alisema Wasira.
Sign up here with your email
