POLISI WACHARUKA NCHINI. - Rhevan Media

POLISI WACHARUKA NCHINI.



Polisi imesema ina taarifa juu ya kuibuka kwa makundi ya kihalifu nchini na imejipanga kukabili wahusika. Aidha, Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, amehadharisha askari na watendaji wa jeshi hilo, aliowataja kuwa wasaliti na kusema watakaobainika watafukuzwa na si kuhamishwa vituo.Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya jeshi katika mapambano ya uhalifu nchini, Marijani amewataka wananchi kuwa watulivu , kutotaharuki kwa kile alichosisitiza kuwa nchi iko salama wakati Polisi ikiendelea kujipanga kukabili vikundi husika.
Kamishna Marijani alisema makundi ya uhalifu yanayoibuka nchini yamekuwa kero . Alisema juhudi za makusudi zinafanywa kuyadhibiti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.“Hatuwezi kuweka mikakati yetu hadharani ya kukabiliana na vikundi vya uhalifu vilivyoibuka hivi sasa, ila wafahamu kwamba tutawadhibiti kikamilifu,” alisema Kamishna Marijani. Alisema hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu bali wawe watulivu na kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali, kwa sababu vyombo vya usalama vipo na vitahakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unalindwa .
Previous
Next Post »