Kiongozi mkuu wa chama cha Former Forum for Democratic Change (FDC) Dk Kizza Besigye amekamatwa leo saa moja kabla ya Bunge kuanza kujadili pendekezo la kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Besigye, aliyewahi kugombea urais mara nne na akishindwa kwa Rais Yoweri Museveni alikamatwa mjini hapa alipokwenda kuwahamasisha wafuasi wake kupinga kufutwa Ibara ya 102 (b) kwenye Katiba iliyoweka ukomo wa kugombea urais kuwa miaka 75.
Besigye alikataa kushuka kutoka kwenye gari lake hali iliyowalazimisha maofisa wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kampala (DPC) wakiongozwa na Joseph Bakaleke kulivuta gari lake hadi kituoni hapo.
Vilevile Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Fred Mukasa Mbidde alikamatwa kuhusiana na suala hilo hilo. Zilikuwepo taarifa za kukamatwa vijana wengi katika maeneo mbalimbali yalikofanyika maandamano ya kupinga pendekezo hilo. Maeneo mengine yalikofanyika maandamano ni Mbale, Arua, Mbarara, Masaka na Pader
Katika hatua nyingine, maofisa polisi walisambazwa katika maeneo mengi muhimu katika jiji la Kampala ulinzi unaohusiana na pendekezo la kufutwa Ibara ya 102 (b) ya Katiba likilenga kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Makao makuu ya ofisi za chama cha FDC yalizingirwa na polisi wa kawaida, wa kuzuia ghasia na wa kupambana na ugaidi. Ofisi hizo zilizopo Najjanankumbi katika barabara ya Kampala-Entebbe zimezungukwa na polisi wenye silaha.
Msemaji wa Polisi Asan Kasingye alisema juzi kwamba maofisa hao wamesambazwa kwa ajili ya kukabiliana na kitisho cha aina yoyote. Kadhalika maeneo mengi nyeti, eneo lililojaa shughuli za kibiashara na Bunge yote yanalindwa.
Polisi wa kijeshi pia wamesambazwa maeneo ya Constitution Square ambako wameweka mahema sawa na bungeni, eneo muhimu kwa ajili ya mjadala uliotarajiwa kuwasilishwa jana kuhusu kuondolewa ukomo wa umri.
Kusambazwa kwa wingi kwa askari hao kumefanyika katikati ya kampeni zinazofanywa na za vikundi vya kisiasa na sasi za kiraia kupinga marekebisho ya katiba yanayolenga kufuta ukomo wa umri wa rais wa miaka 75. Hoja ya marekebisho hayo ilitarajiwa kuwasilishwa jana baada ya kushindikana Alhamisi iliyopita.
Mjadala ni mkali ndani ya bunge na chama tawala cha NRM wakiwemo baadhi ya wenyeviti wa majimbo ambao wamepinga pendekezo la kufuta Ibara ya 102 (b) ya Katiba wakisema ni jaribio la kupindua sheria mama.
Baraza la Viongozi wa Dini nchini limeongeza uzito kwa kutoa wito kwa serikali kuruhusu hoja ya ukomo wa umri wa rais iamuliwe na wananchi wote kwa kupiga Kura ya Maoni.
Baraza hilo linalojumuisha wakuu saba wa madhehebu makubwa ya dini nchini limesema katika taarifa yao ya pamoja wiki iliyopita kwamba watu waruhusiwe kuamua hatima yao.
“Mjadala kuhusu kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais si suala la upande mmoja ambalo linahodhiwa na wanasiasa na au wabunge...wananchi wana maoni tofauti kuhusu sauala hilo, hivyo kuna haja ya kusikiliza kwa utulivu pande zote bila ya kuegemea upande mmoja na kuutisha mwingine.
Hivi karibuni wabunge wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na wa kujitegemea walipitisha uamuzi wa kuondolewa ukomo wa umri wa miaka 75 uliowekwa katika Katiba.
Ikiwa marekebisho hayo yatapitishwa bungeni, itakuwa na maana kwamba Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 sasa ataweza kugombea uchaguzi ujao mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77. Mwaka 2005, katiba ilifanyiwa marekebisho ukaondolewa ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja
Sign up here with your email