FAO YAIPA MBINU TANZANIA YA KUPAA KIUCHUMI - Rhevan Media

FAO YAIPA MBINU TANZANIA YA KUPAA KIUCHUMI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao), Jose Graziano da Silva 



Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao), Jose Graziano da Silva amesema wapo tayari kushirikiana na Tanzania kufanya mageuzi katika kilimo.
Mageuzi hayo yanahusisha uzalishaji wa mazao na viwanda vya kuyachakata ili kuyaongeza thamani.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema hayo jana Septemba 6, Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.
Amemshukuru Rais kwa ushirikiano ambao shirika hilo limeupata kwa kipindi cha miaka 40 ya uwepo wake nchini.
Graziano da Silva amesema Tanzania inaweza kupata manufaa ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kuuza nje ya nchi, kuzalisha ajira na kukuza pato la Taifa kupitia mapinduzi yatakayotokana na kuunganisha kilimo na viwanda, vikiwemo vya kusindika nyama na samaki kwa kuwa fursa zipo nyingi.
Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amemhakikishia kiongozi huyo wa Fao kuwa Serikali itaendeleza na kuimarisha  ushirikiano, akitilia mkazo dhamira yake ya kutaka ushirikiano uelekezwe katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Tanzania ina maziwa mengi, ina ukanda wa bahari wenye urefu wa kilomita 1,422 na ina mito mingi ambayo inaweza kuwekezwa viwanda vya samaki, inashika nafasi ya pili kwa mifugo barani Afrika, hivyo tunahitaji kujenga viwanda vya nyama,” amesema.
Rais Magufuli amesema asilimia 75 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana ambao wana uwezo wa kuzalisha mazao mengi ya kilimo.
“Tunahitaji viwanda, uchumi wetu ni mzuri na unakua kwa wastani wa asilimia 7.1, kwa haya yote tunahitaji wadau ikiwemo Fao tushirikiane kutumia fursa hizi,” amesema. Amesema Serikali imejipanga kusimamia miradi yoyote itakayoletwa nchini ili itekelezwe kwa uadilifu na ubora wa hali ya juu.
0
Previous
Next Post »