KONDA , DEREVA WA DALAALA , WAMSHAMBULIA MFANYAKAZI WA MWANANCHI - Rhevan Media

KONDA , DEREVA WA DALAALA , WAMSHAMBULIA MFANYAKAZI WA MWANANCHI

Tokeo la picha la DALADALA VURUGU ZA KONDA

Moshi. Mwakilishi wa mauzo wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) mkoa Kilimanjaro, Ewald John, ameshambuliwa na kuumizwa vibaya na dereva na kondakta wa basi dogo la daladala aina ya Hiace.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi saa 12:00 katika eneo la Mbwaharuki nje kidogo ya mji wa Moshi, baada ya dereva na kondakta wa daladala hilo kumzuia kushuka kwenye gari hilo na kumshambulia.
"Tulikaa muda mrefu daladala haliondoki tukawalalamikia hawatusikilizi. Nikaamua kushuka nitafute usafiri mwingine ndipo walipoanza kunipiga na kuniumiza," amesema na kuongeza:
"Dereva alitoka upande wake na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa chupa na kitu kizito kichwani na kunichania shati na kuniibia fedha na simu".
Kwa mujibu wa John, katika tukio hilo, ameporwa Sh250,000, saa yenye thamani ya zaidi ya Sh25, 000 na simu yenye thamani ya Sh420, 000.
Hata hivyo amesema, abiria wengine ambao nao walianza kushuka, walichachamaa kupinga kushambuliwa kwake ndipo dereva na kondakta wakaondoa basi hilo kwa kasi.
"Abiria wenzangu na madereva wa bodaboda katika eneo lile walikuwa msaada mkubwa kwangu. Dereva mmoja wa bodaboda ndio alinipa msaada wa kunipeleka polisi,"amesema.
Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alipotafutwa alisema yupo kikaoni lakini mmiliki wa basi hilo, Evod Moshi alikiri kupewa taarifa juu ya tukio hilo.
Moshi amesema alijulishwa kuwa wafanyakazi wake wameegesha basi hilo katika kituo kimoja cha mafuta eneo la Sango na kuelekeza wafanyakazi wa sheli wamjulishe mwenye gari.
"Nimeambiwa waliegesha gari na wakasema kuna soo (shida) wamefanya mahali hivyo hawatabeba tena abiria kwa siku ya leo (jana)," alisema.
Moshi amesema amejaribu kuwapigia simu dereva na kondakta wake baada ya kupokea taarifa hizo lakini simu zao zilikuwa zikiita lakini kwa wakati huo saa 6:00 mchana zilikuwa hazipatikani tena.
Gazeti hili lilishuhudia polisi wa upelelezi wakimchukua mmiliki huyo ili asaidie kupatikana kwa gari hilo pamoja na watuhumiwa wanaodaiwa kutenda kosa hilo.











Previous
Next Post »