KABURU ASHINDWA KUFIKA MAHAKAMANI - Rhevan Media

KABURU ASHINDWA KUFIKA MAHAKAMANI



Dar es Salaam. Makamu Rais wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' ameshindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi kutakatisha fedha na kughushi inayomkabili yeye na rais wa klabu hiyo, Evans Aveva katika Mahakama ya Hakimu  Mkazi Kisutu kwa sababu anaumwa.
Hayo yameelezwa leo asubuhi na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa, (Takukuru), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Julai 31, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Akiiahirisha kesi hiyo, Hakimu Nongwa aliutaka  upande wa serikali kukamilisha upelelezi haraka kwa sababu washtakiwa wapo rumande.
Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha dola 300,000.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakionyesha klabu ya Simba inalipa mkopo wa  dola 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakati akijua ni kosa.
Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata dola  300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kati ya Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia dola 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva  kujipatia dola 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.
Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
Previous
Next Post »