Wakati Serikali na kampuni ya Acacia zikiwa zinajiandaa kwa mazungumzo ya kumaliza mzozo wa usafirishaji mchanga wa madini nje ya nchi, taarifa zinaonyesha timu ya Tanzania itakuwa na kazi ngumu kukabiliana na upande wa pili.
Timu ya kampuni hiyo kubwa ya uchimbaji madini itaundwa na viongozi kutoka kampuni ya Barrick Gold Cooperation na Acacia.
Barrick inamiliki zaidi ya asilimia 63 za hisa za Acacia, ambayo inaendesha migodi ya Buzwagi, Bulyanhulu, inayozalisha mchanga unaosafirishwa nje kwa ajili ya kwenda kuuyeyusha kupata mabaki ya madini, pamoja na North Mara.
Mazungumzo hayo kwa upande wa Barrick yatahusisha vigogo 12 ambao ni wajumbe wa Bodi ya Kimataifa ya Ushauri, ambayo kwa mujibu wa tovuti yao imepewa jukumu la kutoa ushauri kwa Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti kuhusu masuala ya ardhi na siasa na mambo mengine ya kimkakati yanayoathiri kampuni.
Vigogo hao ni pamoja na mawaziri wakuu wawili wa zamani, na mawaziri watatu wa zamani wa nchi nne tofauti zilizoendelea.
Mwenyekiti wa bodi hiyo ni Brian Mulroney, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Canada kati ya mwaka 1984 na 1993, Jose Maria Aznar, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Hispania (1996-2004), pamoja na aliyekuwa spika wa Bunge la Marekani Newt Gingrich (1995-1999) na ambaye pia ni shabiki mkubwa wa Rais Donald Trump ndani ya chama cha Republican.
Wajumbe wengine wazito ni John R. Baird, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada (2011-2015) , William S. Cohen, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani (1997-2001) na Karl-Theodor zu Guttenberg aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani (2009-2011).
Mwingine ni Charles Powell, aliyekuwa mshauri wa mambo ya nje wa Margareth Thatcher (Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na John Major (1990). Kwa sasa Powell ni mjumbe wa Bunge la Mabwenyenye na amekuwa mshauri wa kampuni za Rolls-Royce na BAE Systems.
Wajumbe wengine wa bodi hiyo ni Peter Munk, muasisi na mwenyekiti wa Emeritus, Barrick Gold Corporation, mshauri wa kampuni za Akin, Gump, Strauss, Hauer & Feld na L.L.P, Vernon E. Jordan Jr, Andrónico Luksic na Gustavo Cisneros, mwenyekiti wa Cisneros Group of Companies ya Jamhuri ya Dominica.
Mwenyekiti mtendaji wa Barrick, Profesa John Thornton, ambaye alikutana na Rais Magufuli Jumatano na kukubaliana kuanza mazungumzo ya kumaliza mzozo wa suala hilo, pia ni mjumbe wa bodi hiyo.
Kwa upande mwingine, bodi ya Acacia inaundwa na watu wanane, akiwemo Mtanzania Juma Mwapachu, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mwenyekiti wa bodi hiyo ni Kelvin Dushnisky ambaye pia ni Rais wa Barrick. Mjumbe mwingine ni ofisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Brad Gordon.
Wakati Rais Magufuli alisema baada ya kukutana na Profesa Thornton kuwa Acacia imekiri makosa na imekubali kulipa deni, kampuni hiyo juzi usiku ilitoa ufafanuzi kuwa licha ya kukubaliana kuingia katika mazungumzo, “hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa, lakini mazungumzo yatalenga kutafuta suluhisho kwa ajili ya maslahi ya pande zote mbili”.
Credit - Mwananchi
Sign up here with your email