THERESA MAY ' HANA NIA ' YA KUJIUZULU LICHA YA KUTOFANIKIWA UCHAGUZINI UINGEREZA - Rhevan Media

THERESA MAY ' HANA NIA ' YA KUJIUZULU LICHA YA KUTOFANIKIWA UCHAGUZINI UINGEREZA

Theresa May wakati wa kuhesabiwa kwa kura eneo lake la Maidenhead

Haki miliki ya pichaPA
Image captionTheresa May wakati wa kuhesabiwa kwa kura eneo lake la Maidenhead
Uingereza inakabiliwa na uwezekano wa kuwa na bunge la mng'ang'anio, ambapo hakuna chama chochote kilicho na ubabe, baada ya chama kikubwa zaidi nchini humo cha Conservative kushindwa kupata wingi wa wabunge uchaguzini Alhamisi.
Baada ya matokeo kutoka maeneo mengi kutangazwa, Theresa May anapungukiwa na wabunge 12 ukilinganisha na wabunge aliokuwa nao wakati wa kuitisha uchaguzi huo.
Chama chake kinaelekea kupata wabunge 319, Labour chake Jeremy Corbyn wabunge 261, SNP 35 na Lib Dems 12.
BBC imefahamu kwamba Waziri Mkuu Theresa May hana nia ya kujiuzulu na kwamba atajaribu kuunda serikali.
Lakini Jeremy Corbyn amesema pia kwamba yuko "tayari kutumikia".
Bi May amesema taifa hilo linahitaji uthabiti baada ya matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hayakuonesha nani mbabe.
Mhariri wa masuala ya siasa wa BBC Laura Kuenssberg amesema Bi May anakusudia kujaribu kuongoza wka msingi kwamba chama chake kilipata idadi ya juu zaidi ya kura na wabunge wengi.
Lakini kumekuwa na uvumi kwamba huenda akatafuta aina fulani ya ushirikiano na chama cha Democratic Unionists, ambacho kilishinda viti kumi Ireland Kaskazini.
Chama cha Conservatives kinatarajiwa kupata 42% ya kura zote, Labour 40%, Lib Dems 7%, UKIP 2% na Greens 2%.
Baada ya Corbyn kupata matokeo mazuri kuliko ilivyotarajiwa, Labour wanatarajiwa kupata viti 29 zaidi ya walivyokuwa navyo.
Conservatives watapoteza viti 13. Chama cha SNP nacho kitapoteza viti 22, ambavyo vimetwaliwa na Conservative, Labour na Lib Dems, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa kiongozi wa chama hicho Nicola Sturgeon.
Idadi ya waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo wa Alhamisi kufikia sasa ni 68.7% - juu na 2% ukilinganisha na 2015 - lakini uchaguzi huo umepelekea kurejea kwa siasa za vyama viwili katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Vyama vikuu viwili - Conservative na Labour - vimepata idadi kubwa ya kura kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1990.
Chama cha UKIP kilipoteza kura nyingi , lakini badala ya kura hizo kuendea chama cha Conservative kama walivyotarajia, wapiga kura wengi waliokuwa wanaunga chama hicho walihamia chama cha Labour.
Bw Corbyn, akizungumza baada ya kuchaguliwa tena Islington North, alisema wakati umefika kwa Bi May "kufungua njia2 kuwezesha kuundwa kwa serikali ambayo itawakilisha kikamilifu maslahi ya nchi hiyo.
Graph
Baadaye, aliambia BBC kwamba ni wazi kabisa nani alishinda uchaguzi huo.
"Tuko tayari kuwatumikia wananchi ambao wameweka imani yao kwetu," alisema, lakini akasisitiza kwamba hataingia kwenye mkataba na vyama vingine.
Chama cha Conservatives kimesema iwapo kutakuwa na bunge la mng'ang'anio atapata nafasi ya kuunda serikali kwanza, kama ilivyofanyika mwaka 2010 mtangulzii wake David Cameron alipokosa wingi wa wabunge.

Mada zinazohusiana

Previous
Next Post »