Ikiwa mishahara ya wachezaji soka inaongezeka na mahitaji ya wachezaji nyota wa soka yakiwa ni mamilioni ya shilingi, klabu nyingi sehemu mbalimbali duniani zimekuwa zikiwaendeleza vijana katika shule zao za soka ili kupunguza kununua wachezaji kwa mamilioni ya fedha.
Inafahamika kwamba kwa muda mrefu sasa klabu nyingi barani Ulaya zimekuwa zikitumia wachezaji waliotokana na akademia zao na hivyo kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali. Pia klabu nyingine zimekuwa zikiwaandaa wachezaji vijana wengi katika akademia zao na kuwauza.
Kwa hiyo klabu inapokuwa na akademia ya soka huwa na nafasi ya kuandaa wachezaji na kuwamiliki au kuwauza na kupata fedha kwa maendeleo ya klabu yao. Pia, biashara ya akademia ni nzuri vile vile kwa watu binafsi wenye uwezo kama wakiamua kuwekeza katika biashara hii ya akademia za soka.
Kuna uzuri mbalimbali wa akademia za soka, kwa mfano akademia inaweza ikawa inatoa na elimu ya shule ya kawaida ili wale wachezaji watakaoshindwa kufanikiwa kuendelea na soka la kulipwa waendelee na shule mpaka chuo kikuu na baada ya hapo wapate kazi ya kufanya itakayowasaidia katika maisha yao. Akademia inaweza ikawa na timu za U-18, U-16, U-15, U-14, U-13, U-12, U-11, U-10 na U-9.
Kwa klabu ambazo zinaelewa na zina falsafa nzuri ya soka huwatambua wachezaji bora katika akademia zao na klabu zao kwa ujumla, tena wa umri tofauti na hawawauzi, kwani kama unataka klabu yako iwe bora duniani, usijaribu na wala usifikirie kuuza wachezaji wako bora.
Klabu inatakiwa kuwa na uwezo wa kuwamiliki wachezaji wao bora kama inataka mafanikio, inatakiwa izionyeshe klabu nyingine kwamba falsafa yao si kuuza wachezaji bora ila ni kununua wachezaji bora tu kutoka klabu nyingine tena pale inapobidi kufanya hivyo ili kupunguza kununua wachezaji kwa mamilioni ya fedha.
Viongozi wa klabu pamoja na kocha wao wanatakiwa kuwa na falsafa nzuri, kwamba wawe watulivu wakati wa usajili na wanunue wachezaji bora, hivyo wakinunua wachezaji bora ndani ya miaka kadhaa wataanza kuona mwelekeo wa mafanikio bora na kuwa na timu imara.
Hapa ninamaanisha kwamba viongozi wa klabu pamoja na kocha wao wanatakiwa kufikiria kitu kimoja tu, ambacho ni kujenga klabu ya soka. Kama unataka kujenga klabu ya soka lazima ukubali kuanzia chini. Hatahivyo, makocha asilimia 99 wakipewa kazi huwa wanafikiria kwanza ushindi ili wasitimuliwe. Kwa hiyo wananunua wachezaji wa haraka haraka na wenye uzoefu. Katika klabu nyingine ukifungwa mechi tatu mfululizo unatimuliwa. Dunia ya soka la sasa ambalo linaongozwa na viongozi wanaotaka faida ya haraka, sina uhakika kama wataweza kuwa na uvumilivu wa kumsubiri kocha aijenge timu kwa zaidi ya miaka minne.
Ikumbukwe kwamba, kushinda mechi ni mafanikio ya muda mfupi, unaweza ukapoteza mechi inayofuata. Kujenga klabu inaleta uthabiti na msimamo. Kuna wachezaji wa hatua tatu tofauti: kwanza wachezaji wenye umri wa miaka 30 na kuendelea, wachezaji wa miaka 23 mpaka 30 na wachezaji wa miaka 23 kushuka chini.
Dhamira kubwa ni kwamba wachezaji wenye umri mdogo wanakuwa kwenye timu na watakuta viwango ambavyo wachezaji wakubwa wameweka.
Kocha na viongozi wa timu wanatakiwa kuelewa kwamba mzunguko wa wachezaji na timu kupata mafanikio huwa kwa miaka minne na baada ya hapo mabadiliko yanahitajika.
Kwa hiyo kocha na viongozi wa timu wanatakiwa kuitazama timu yao ndani ya miaka mitatu au minne na baada ya hapo wanatakiwa kufanya uamuzi wa kusajili wachezaji bora wengine katika nafasi tofauti.
Ninachokiona kinachofanyika hapa nyumbani wakati wa usajili kwa zaidi ya miaka 20 huwa ninashangaa sana, kwani tumekuwa tukishuhudia ujio wa nyota mbalimbali wa kigeni wanaomiminika nchini kwa ajili ya kuja kucheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa za soka Tanzania, lakini nyota hao huonyesha kiwango cha chini na husajiliwa na kulipwa fedha nyingi.
Unajua hapa nchini viongozi wa soka na baadhi ya makocha wanasahau kuwa soka ni mchezo unaochezwa hadharani, hivyo mchezaji akisajiliwa na kuonyesha kiwango cha chini watamtupia virago, atakuwa ameipotezea muda timu na atakuwa ameshindwa kuiletea mafanikio timu.
Tatizo kubwa ninaloliona ni kwamba, klabu zetu hazina wang’amuzi wa vipaji wa kuwafuatilia wachezaji nje na ndani ya nchi, pia, usajili wa wachezaji wa kigeni na wale wa ndani unafanywa na kila mtu na hivyo kuletwa hata wasio na sifa ili tu kuzuga mashabiki.
Hapa wanasajiliwa kwa mbwembwe na fedha nyingi, lakini wanacheza msimu mmoja tu chali, baada ya hapo wanapigwa chini na unafanyika usajili mwingine wa wachezaji ambao nao pia hushindwa kuonyesha soka la kiwango cha juu. Tuendeleze vijana wetu.
Sign up here with your email