Titi la Mama ni tamu. Hata likiwa la mbwa. Kiswahili naazimu. Sifayo inayofumbwa. Niimbe ilivyo kubwa. Toka kama chemuchemu.Titi la Mama litamu jingine haliishi hamu. Aliwahi kuandika hayati Shaban Robert katika moja ya vitabu vyake.
Nimemaliza kufuturu hapa kwa mama Dunia. Futari yake imenikumbusha mbali sana. Tangu mwezi uanze hii ndiyo futari yangu ya kwanza kwa mama yangu. Futari yake imenikumbusha hayo maneno magumu ya nguli huyo. Shaban Robert ni kati ya waandishi walitokea kunivutia kutokana na kalamu yake anapoitumia. Hakuna kama Shaban Robert. Acha niishie kusema hivyo.
Baada ya kushiba futari nimekaa na zile kaseti mbili za Azam TV. Moja kwenye mechi kati ya Simba na Mbeya City. Nyingine Yanga na Ruvu Shooting. Zote za msimu uliopita.
Nimetazama kaseti hizo na nimezielewa. Nimeona wachezaji wawili tu. Kwanza nimemuona Ibrahim Ajab alafu nimemalizia kumuona Haruna Niyonzima maarufu kama Fabregas. Hao tu ndio niliowaona katika mechi hizo.
Kufananishwa na mtukama Fabregas sio jambo dogo kabisa. Lazima uwe na kitu cha ziada ile kweli ufananishwe naye. Si mlimuona yule Idrisa maarufu kama Ronaldo wa Misosi Fc. Kapiga tano pekee yake. Hakika anafaa kuitwa Ronaldo.
Nimemuona Ajibu akifunga bao la kusawazisha kwa faulo ya moja kwa moja. Kisha nimemuona Niyonzima akiimaliza Ruvu Shooting kwa pasi yake murua iliyomfanya mmoja wa mabeki kuanguka kama mzigo wa karanga. Mwisho nimemuona Niyonzima akimvisha kanzu beki. Ghafla nikaikumbuka ile kanzu ya Zinedine Zidane dhidi ya Ronaldo De Lima mwaka 1998.
Kuna vitu wanavyojaribu kuvifanya wachezaji hawa, sio vya kwenye Ligi yetu kabisa. Hakika tumewahi kuwashuhudia watu wakila kanzu miaka ya nyuma sana. Zama za kina Method Mogela na Athuman Chama ndio kipindi cha watu walipokuwa wakipigwa kanzu sio kipindi hiki cha sasa. Tuachane na hilo.
Mwishoni mwa wiki hii kuna taarifa zilizoenea kuwa Ajibu amesaini Yanga. Leo kuna mtu ameniambia kuwa Niyonzima amesaini Simba. What a football?
Huu ndio mpira wa kweli. Niyonzima Simba alafu Ajib Yanga. Ni nadra sana katika Ligi moja wachezaji muhimu kuondoka ndani ya msimu mmoja huku wakibadilishana timu. Hakika ni mara chache sana kwa tukio kama hili.
Katika moja ya maandiko ya mzee Arsenal Wenger aliwahi kusema kuwa ‘Footballer is Most Hypocrite people in the world” akiwa na maana kuwa wachezaji ni moja kati ya watu wanafiki duniani. Tuliamini kama moyo wa Niyonzima utapokea kelele za mashabiki wa Simba? Akili ya Ajibu itakubali lawama za Simba? Kila kitu acha kimalizike lakini mpira uwepo kwanza.
Hapo awali mashabiki wa Simba wa.limzomea Niyonzima. Yanga wakamzomea Ajib. Lakini leo. Kila mmoja anakaribisha wa kwake. This is Football and Football is Fair Play Game. Naanza kuiamini FIFA ilipotueleza hilo.
Kama Torres alikubali kutoka Liverpool kwenda Chelsea. Raul Meireles pia. Ajib anaachaje. Niyonzima anaachaje? Huu ndio unafiki aliouzungumzia Wenger. Ronaldo anamapenzi na United lakini alikwenda Real Madrid. Huwezi kuzuia pesa kwa moyo wa mapenzi. Steven Gerard hadi leo bado anajaribu kujifariji kwa dhambi aliyoifanya mwaka 2005.
Gerard kwenye ubora wake. Liverpool inatwaa UEFA pale Instanbul. Real Madrid, Barcelona na FC Bayern Munich zinamtaka. Alichokifanya ni kuweka mapenzi na Liverpool. Akapoteza alichoandikiwa kukipata. Anyway tuje kwenye mada muhimu.
Ajibu anakwenda kuikosa akili ya Niyonzima. Niyonzima anakwenda kuikosa miguu ya Ajibu. Najaribu kufikiria kama wawili hawa wangekuwa kwenye timu moja. Hakika hakuna zaidi ya kupigiwa mpira mwingi. Hakuna zaidi ya hicho.
Hebu jaribu kufikiria zile Auta za Ajib na Chenga za Niyonzima. Umakini wa Ajib na pasi za Niyonzima. Mizuungusho ya Ajib na ufundi wa Niyonzima. Ukiwa na watu hawa kwenye timu humuitaji tena Ngoma wale Tambwe. Chirwa mmoja anakutosha.
Kuwa na watu kama Niyonzima na Ajibu kwenye timu moja. Huitaji uwepo wa Mavugo wala Blagnon. Waziri Junior ama John Bocco tu wanakutosha. Hakika wanakutosha.
Jaribu kufikiria zile chenga za Ajibu na kanzu za Niyonzima na ule utimamu wa Chirwa wakiwa kwenye timu moja. Najaribu kuufikiria uwezo wa ‘Mo’ Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajib wakiwa kwenye timu moja. Hakika niliwahi kuomba itokee hii lakini imekuwa ngumu kidogo.
Unaachaje kujisifu unapokuwa na Ajib na Niyonzima kwenye timu yako. Uwepo wa Ajib na Niyonzima ni sawa na ule uwepo wa Zidane na Ronaldo pale Real Madrid. Chenga utapigwa na kufungwa utafungwa tu. Hakika this is football.
Watu hawa wamekosana. Vipaji vyao vimekosana. Uwepo wao pia umekosana. Katika vitu ambavyo nafikiria Ajib na Niyonzima walitakiwa kuviomba nikuwa kwenye timu moja. Lakini imekuwa ngumu kwao.
Acha nizirudishe hizi kaseti kwenye kabati maana machozi yameshaanza kunilenga. Napomuangalia Ajib alafu Niyonzima naona ule uwepo wa Christiano Ronaldo na Wayne Rooney. Manchester United ikitwaa UEFA dhidi ya Chelsea.
Sign up here with your email