Iringa. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuwadhibiti maofisa watendaji wa vijijiji na kata ambao wamekuwa wakitafsiri tofauti maagizo ya viongozi na kufanya maamuzi yanayowaumiza wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha siku moja kilichowakutanisha wabunge wa mkoa wa Iringa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa na wilaya zote pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa na madiwani, alisema maamuzi yao yamekuwa yakiwalazimu wananchi kuichukia Serikali na CCM.
Kikao hicho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kutoa msimamo na mapendekezo ya Serikali kuhusu kilimo cha umwagiliaji kinachofanywa kwenye maeneo yaliyokaribu na vyanzo vya maji lengo likiwa kuokoa uharibifu wa vyanzo hivyo.
“Ninaomba mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote mpo hapa, muwadhibiti watendaji wa vijiji na kata ambao wanakuwa na tafsiri zao binafsi kuhusu maelezo ya viongozi, wakati mwingine wanatuharibia sisi Serikali au sisi tunaovaa jezi za kijani wana CCM,” alisema Makamba.
“Wamekuwa wakiweka mambo yao na kuongeza vitu vyao, ukali wao ambao hauna sababu yoyote na wakati mwingine kutunga faini ambazo hazipo katika utaratibu na pia huwa na mahakama zao wanakuwa wao ndio waendesha mashitaka na mahakimu, nawasihi muwaite watendaji na muwaeleza na yule atakayeendesha jambo hilo kinyume na utaratibu achukuliwe hatua,”alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masena alisema hakuna mtendaji atakayepona endapo atagundulika kutekeleza shughuli za serikali kinyume na utaratibu.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kuwataka wale waliokwishalima maeneo yaliyokaribu na vyanzo vya maji kuendelea na shughuli zao hadi hapo Serikali itakapokamilisha mchakato wa kutambua na kubaini maeneo yanayostahili kuachwa.
Sign up here with your email