Sengerema. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Eliud Mwaiteleke kuitisha kikao na wananchi wa Kigongo kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga soko. Ametoa agizo hilo leo Jumatano jioni wakati akizungumza na mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia Kivuko cha Kigongo waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.
“Mkurugenzi haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko eneo hili ili waweze kuuza mazao yao au samaki?" alihoji Majaliwa na kuongeza:
"Ninakuagiza mkurugenzi, kesho Alhamisi saa nne njoo na ofisa biashara wako, mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na diwani wa hapa, itisheni kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango yenu."
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.
Pia, Waziri mkuu alimwita mkurugenzi huyo ili aeleze namna alivyojipanga kwenye halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.
Akitoa majibu, Mwaiteleke amesema hawajawahi kupata mpango kutoka kwenye kata hiyo hivyo akawasihi wananchi waibue mpango huo na kuuwasilisha kwenye halmashauri ili waweze kutengewa fedha.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Sebastian Kisumo alimweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko na uhaba wa maji.
Kuhusu maji, Majaliwa amesema Serikali imetenga Sh2.5 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao utasambaza huduma hiyo Misungi, Usagara hadi Kigongo Feri.
Habari
Sign up here with your email