MAANDALIZI YA AFCON U-17 - 2019 YAANZA MAPEMA - Rhevan Media

MAANDALIZI YA AFCON U-17 - 2019 YAANZA MAPEMA

Tokeo la picha la AFRICON U 17



Tanzania itaandaa Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, baada ya kukabidhiwa uenyeji na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika hafla iliyofanyika wiki chache zilizopita nchini Gabon.
Hatua hiyo itamaliza kiu ya muda mrefu ya Tanzania kuandaa michuano iliyo chini ya CAF.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa fainali hizo za soka Afrika tofauti na mataifa mengine kama Rwanda, Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, Misri na Angola ambayo yameandaa mara kadhaa fainali hizo na zile za wakubwa.
Mashindano hayo yaliyoasisiwa miaka 32 iliyopita, hufanyika kila baada ya miaka miwili na Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka huu ilishiriki fainali hizo zilizofanyika nchini Gabon na kuishia katika hatua ya makundi.
Kuandaa michuano mikubwa kama hii kunahitaji maandalizi ya mapema na ya uhakika ambayo yatashirikisha Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wakiwemo wafadhili.
Tumeshuhudia uwezo uliionyeshwa na timu shiriki za Ghana, Mali, Guinea na Niger katika fainali zilizofanyika Gabon na kufanikiwa kupata tiketi za kuliwakilisha bara la Afrika kwenye fainali za dunia zitakazofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.
Kuandaa tu michuano hakutoshi kukuhakikishia kufanya vizuri, tumeona namna Gabon ilivyotia aibu baada ya kuandaa fainali hizo lakini timu yake iliishia kufungwa jumla ya magoli 10 katika mechi tatu za hatua ya makundi na kuondolewa mapema kwenye fainali hizo.
Lazima tujidhatiti kutengeneza timu imara ambayo itaweza kupambana na mataifa ya Afrika Magharibi ambayo yamepata mafanikio makubwa kwenye michuano hii na jitihada hizo hazitazaa matunda kama wadau wote hawatakaa pamoja.
TFF kwa upande wake imeshaanza taratibu za kuandaa timu itakayoshiriki fainali hizo ambapo mpango wa awali ulikuwa kusaka wachezaji na kuwaweka pamoja mkoani Mwanza. Pia TFF inaweza kutumia michezo ya shule za sekondari yaani Umisseta inayoanza kesho jijini Mwanza na baadaye yale ya shule za msingi yaani Umitashumta ili kusaka wachezaji watakaoongezwa kikosini.
Jukumu la TFF ni kuhakikisha benchi la ufundi linafanya kazi yake kwa kuwa na kambi imara ili kuandaa timu imara ambayo itakuwa na uwezo wa kubakiza kombe nyumbani. Maandalizi hayo yahusishe kucheza mechi za kirafiki na program za mara kwa mara za mazoezi.
Najua kwa sasa viongozi walioko TFF nao wanataka kuendelea kuwa viongozi, wanapigana usiku na mchana ili kubaki madarakani lakini muda hautusubiri. Jitihada zilizotumika kuiandaa Serengeti Boys iliyoshiriki michuano ya Gabon zinatakiwa kuongezewa nguvu ili kuiandaa Serengeti ya 2019.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singu aliliambia gazeti hili wiki iliyopita kuwa hivi karibuni, Serikali itaunda kamati ya kitaifa ya maandalizi itakayojumuisha maofisa wa idara ya uhamiaji na usalama ambayo itatoka na mapendekezo mbalimbali yakayotatumika kuunda kamati ndogondogo za kitaalamu kwa ajili ya kufanikisha maandalizi kuelekea michuano hiyo.
Aidha, Singu alisema Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya SportPesa, hivi karibuni itaanza kuufanyia marekebisho Uwanja wa Taifa hususani katika eneo la kuchezea na vyumbani, lengo likiwa ni kuhakikisha uwanja huo unakuwa vizuri muda wote kabla na wakati wa fainali hizo zitakazopigwa mapema 2019.
Ni vyema hatua zote hizi zikachukuliwa mapema ili kamati ndogondogo ziundwe haraka na kuanza kazi ya kutayarisha miundombinu.
Tukifanya vyema, tutapata heshima hata ya kuandaa fainali za CHAN na baadaye fainali za Afrika (Afcon).







Previous
Next Post »