Na Regina Mkonde
Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wamelaani kitendo cha serikali ya mkoa wa Kilimanjaro cha kuzuia uwanja wa Mashujaa kutumika kwa ajili ya ibada ya kuaga mwili wa marehemu Philemon Ndesamburo, na kudai kuwa kililenga kuendeleza chuki ya kisiasa.
Katika hatua nyingine, wameshangazwa na CCM kutokuwa na muwakilishi katika ibada ya kuuga mwili wa Ndesamburo aliyefariki dunia wiki iliyopita wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi.
Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa alisema kitendo hicho kimelenga kudhibiti demokrasia. “Nawapongeza kwa maandalizi haya. ila kwa hili inaonyesha jitihada za kudhibiti demokrasia zinaendelea, watu hawa ni wa kuwasamehe bure."
Naye mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Pwani, Fredrick Sumaye alisema “Hata njia za kupitisha maiti nazo zinalindwa hizi chuki tukiacha zijengwe hatutakua hai, wananchi hatutaweza kuwaonea muda mrefu. Ila mbegu ya amani aliyoipanda Ndesamburo itaendelea kuzaa aliyoyasimamia.”
Wakati akitoa salamu hizo, Mwenyekiti mwenza wa UKAWA, James Mbatia alisema kitendo cha viongozi wa CCM kutohudhuria kwenye ibada hiyo si cha kiungwana kwani kinalenga kugawa wananchi kwa misingi ya vyama.
“Walichofanya leo sio cha kiungwana, watanzania tusikubali kugawanyishwa kwa misingi ya imani wala vyama, sijauona uwakilishi wa CCM, tuwasamehe na mimi nimewakilisha CCM wote hapa ili tulete amani ya mzee Ndesa.Ndesamburo alikuwa analeta watu wote pamoja, lakini leo hata njia za kupitisha mwili wake nazo zinalindwa hizi chuki tukiacha zijengwe hatutakua hai,” alisema.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti CUF Severina Mwijage wakati akitoa salamu za rambirambi alisema amesikitishwa na kitendo cha kuzuiwa uwanja kwani marehemu Ndesamburo alishiriki kuujenga uwanja huo.
“Siasa za sasa hivi ni hatari, za kupandikiza watu chuki ni mbaya sana, na mimi naomba niongezeee wenyewe wanajua chuki ndio chama chao kitakachosaidia kuchukua dola, sisi tunachaguliwa na wananchi tunajua matatizo ya wananchi, aelewe yule anayewachonganisha itakuaje yeye ambaye aliyemchagua atakuja na kuondoka na yeye atabaki katika mkoa na watoto wake wanaishi na wananchi,” alisema.
Sign up here with your email