Mshambuliaji huyo wa tatu katika shambulio lililotokea mwishoni mwa juma eneo la London Bridge, Uingereza, ametajwa kama Youssef Zaghba mwenye asili ya asili ya Morocco na Italia.
Mzaliwa wa Pakistan Khuram Butt aliye na umri wa miaka 27, na Rachid Redouane mwenye umri wa 30 ambao wote wawili ni wa kutoka katika eneo la Barking, walikuwa miongoni mwa washambulizi wa tukio hilo.
Wakati huo huo, mhasiriwa mwingine ametajwa kama Kirsty Boden, ambaye ni muuguzi kutoka Australia, mwenye umri wa miaka 28, ambaye familia yake imesema kuwa alikuwa amekimbia akielekea katika daraja hilo kuwasaidia watu.
Watu saba waliuwawa na 48 kujeruhiwa katika shambulio hilo la Jumamosi usiku ambapo washambuliaji hao watatu walipigwa risasi na kuuliwa na polisi.
Zaghba, Butt na Redouane waliwagonga watu waliokuwa wanatembea kwa miguu katika daraja la London, wakitumia gari walilolikodisha majira ya saa tano na dakika 58 usiku, saa za Afrika Mashariki, kisha wakashuka na kuwadunga visu watu wengi katika eneo lililokuwa karibu na soko la Borough.
Maafisa waliokuwa wamejihami kwa silaha waliwauwa wote watatu dakika 8 baada ya kupokea wito wa dharura.
Katika matukio mengine:
- Waziri muu Bi Theresa May, amesema kuwa anatarajia uchunguzi wa wataalamu, utazinduliwa na polisi pamoja na vyombo vya usalama kufuatia shambulizi hilo licha ya kuwepo malumbano kuhusu idadi ya polisi.
- Idara tya Polisi wa katikati wa jiji la London, inasema kwamba mshukiwa mwenye umri wa miaka 27, alishikwa katika eneo la Barking siku ya Jumanne kuhusiana na uchunguzi.
- Msako pia ulifanywa na polisi katika nyumba iliyo katika eneo la Ilford, mashariki mwa London, mwendo wa saa tisa unusu masaa ya Afrika Mashariki, lakini hakuna aliyeshikwa, polisi walisema.
- Charles Phillip na Camilla Rosemary kutoka jamii ya kifalme jijini London watawatembelea manusura katika hospitali ya Royal London.
- NHS England inasema watu 36 wangali wamelazwa hospitalini, 15 kati yao wakiwa katika hali mahututi.
- Ukimya wa dakika moja kwa taifa zima ulifanyika ili kuwakumbuka waliouwawa
- Washukiwa wote 12 walioshikwa siku ya Jumapili baada ya shambulio hilo wameachiwa huru bila kushtakiwa.
Polisi walijua nini kumhusu Khuram Butt?
Kundi linalojiita Islamic State (IS), limesema kuwa "wapiganaji wake" walitekeleza shambulio hilo.
Duru kutoka kwa polisi nchini Italia zimethibitishia BBC kuwa Zaghba, ambaye alikuwa akiishi mashariki mwa London, amekuwa katika orodha ya uchunguzi wa wapelelezi, ambayo husambazwa kwa mataifa mengi likiwemo Uingereza.
Mnamo Machi mwaka 2016, afisa mmoja wa usalam nchini Italia, alimsimamisha Zaghba katika uwanja wa ndege wa Bologna na kumpata na baadhi ya vitu vinavyohusiana na IS kwenye simu yake ya mkononi na akazuiwa kuendelea na safari yake kuelekea mjini Istanbul.
Butt alishirikishwa katika filamu iliyofanywa na Channel 4 mwaka jana kuhusu waislamu wenye itikadi kali walio na uhusiano na mhubiri aliyefungwa Anjem Choudary iliyoitwa "The Jihadis Next Door".
Butt ambaye ameoa na ni baba ya watoto wawili, alipokea mafunzo kama msaidizi wa kutoka huduma kwa wateja London Underground kwa takriban miezi sita mwaka jana, anaonekana kwa filamu akibishana na polisi mitaani,baada ya kuonyesha bendera inayotumika na linalotajwa kama "Islamic State" katika bustani moja jijini London.
Watu wawili katika eneo la Barking, mashariki mwa London, pia walikuwa wameelezea wasiwasi wao kumhusu Butt, mwanahabari wa BBC wa masuala ya ndani ya uingereza, Dominic Casciani alisema.
Mtu mmoja alipiga simu katika kitengo cha kupambana na ugaidi mwaka wa 2015, na mwanamke mmoja alienda kwa polisi kwa kuhofia kwamba Butt alikuwa akiwafunza wanawe itikadi kali.
Naibu mkuu wa Polisi wa Metropolitan Mark Rowley alisema uchunguzi wa Butt ulianzia mwaka wa 2015, lakini "hakukuwa na habari ya kindani kuonyesha kuwa shambulizi hili lilikuwa linapangwa na uchunguzi ulipewa kipao mbele ilivyofaa"
Alipoulizwa ikiwa ulikuwa uamuzi mbaya, bwana Rowley alisema hakuona chochote cha kubainisha hayo.
Manusuru ni akina nani?
Kuna takriban uchunguzi 500 ya visa vya ugaidi yanayohusu watu 3,000 wanaoshukiwa kuhusika.
Bwana Rowley alisema kuwa kazi ilikuwa inaendelea ili kuelewa mengi kuhusu washambuliaji hao, "wanaohusiana nao na iwepo walisaidiwa na watu wengine".
Redouane alikuwa mpishi aliyetumia jina Rachid Elkhdar na polisi walisema alidai kuwa wa asili ya Morocco na Libya. Alimuoa mkewe ambaye ni muingereza jijini Dublin mwaka wa 2012 na kuishi mjini Rathmines.
Kwa sasa tatu kati ya waliouwawa katika shambulizi hilo wametajwa.
Bi Boden alifanya kazi kama muuguzi katika hopitali za Guy na St. Thomas jijini London. Familia yake imemtaja kama alipenda kuzuru kwengi na mkarimu " Tunamsherekea Kristy kwa ujasiri wake ambayo yaonyesha alivyojali watu, sio kwa usiku huo pekee, lakini katika maisha yake yote" waliongeza
Hospitali alikofanyia kazi ilisema kuwa Bi Boden alikuwa muuguzi wa kipekee aliyefaa sana katika vyumba vya kupona baada ya upasuaji.
Mwenyeji wa Canada Chrissy Archibald, mwenye umri wa miaka 30, alikuwa nusura wa kwanza kutajwa. Familia yake inasema kuwa alifariki katika mikono ya mchumba wake baada ya kugongwa na gari la washambulizi hao lilipopita kwa kasi.
Nayo famili ya James McMullan, mwenye umri wa miaka 32 kutoka eneo la Hackney, Mashariki mwa London, wmeisema kuwa wanaamini pia yeye alifariki.
Dadake McMullan anaaminika kuwa kati ya waliofariki, baada ya kadi yake ya benki kupatikana kwa mwili mmoja katika eneo la tukio.
Mfaransa mmoja pia aliuwawa kwenye shambulizi hilo, kulingana na waziri wa kigeni Jean-Yves Le Drian.
Polisi wametoa nambari 0800 096 1233 na 020 7158 0197 za kupigwa na familia na marafiki walio na wasiwasi kuhusu jamaa zao
Sign up here with your email