KIGOGO WA ' UNGA ' AGHARAMIA MAGARI YA SERIKALI ( 3 ) - Rhevan Media

KIGOGO WA ' UNGA ' AGHARAMIA MAGARI YA SERIKALI ( 3 )

Vibanda vinayotumika kuuza mihadarati upande wa
Vibanda vinayotumika kuuza mihadarati upande wa baharini nyuma ya kituo cha basi cha Posta ya Zamani. Vibanda hivyo ambavyo mateja huviita maabara hutumika pia kama sehemu za kutoa huduma ya kujidunga sindano za dawa za kulevya na kuchanganya cocaine na heroin na bangi au sigara kabla ya kuuza au kutumia. Picha Mpigapicha Wetu 
Jana katika mfululizo wa makala zetu za uchunguzi kuhusu usiri uliogubika biashara ya dawa za kulevya nchini, tulitambua baadhi ya maeneo sugu kwa biashara hiyo na mbinu zinazotumika na wauzaji kuficha dawa hizo.
Katika makala ya leo, Kamishna wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rodgers Sianga anaeleza jinsi baadhi ya viongozi wa serikalini na dini wanavyotumika kuwalinda wauzaji wakubwa dawa za kulevya.
Anaeleza pia jinsi baadhi ya wauzaji waliofungwa wanavyoishi maisha ya kifalme gerezani kwa kutumia nguvu ya fedha. Kwanza Mwandishi Wetu anamalizia ziara yake eneo la Mabanda Saba. Endelea…
Eneo la Mabanda Saba lina shughuli nyingi na tulitumia siku nzima kuangalia biashara inavyofanyika.
Eneo hilo ni moja ya maeneo sugu na maarufu kwa utumiaji na biashara ya dawa za kulevya.
Wakati akiendelea kunifunulia jinsi biashara ya mihadarati inavyofanyika, nilimuona kijana akicheza muziki, akiwa amevalia kaptula nyekundu iliyochanika upande wa makalio na shati nyeupe. “Yule kijana niliyekwambia alikuwa akiiba unga wa baba yake ambaye ni kigogo serikalini na kuja kutuuzia, ndiye huyo hapo. Ukimuona unadharau lakini ni mtoto wa kigogo, huyo alishatoroka kwao muda mrefu sana,” anasema Mashikolo.
“Baba yake na ndugu zake wamemfuatilia sana na kuna wakati baba yake alikuwa anakuja hapa na kutupa pesa ili tumkamate, lakini mtoto mwenyewe haambiliki. Akifikishwa nyumbani anatoroka. Ndugu zake wenyewe wamekata tamaa.“Mara ya mwisho, mdogo wake alikuja mwaka juzi kumtafuta, na akaacha maelekezo kwamba akipatikana tumjulishe, lakini mshikaji mwenyewe kama unavyomuona kapinda. Hapo alipo kalewa kinoma.”
Nilimuomba Mashikolo aniruhusu nizungumze naye, lakini akasema akiwa amelewa ni vigumu kuelewana naye na pia huwa mkorofi, hivyo kushauri nimvizie akiwa hajalewa.
“Wewe si umesema unataka kuona unga subiri nikuonyeshe,”anasema Mashikolo, kisha ananyanyuka na kurudi eneo ambalo walikaa mateja na wanauza unga na bangi. Anamwambia kijana mmoja ambaye alimtaja kwa jina kuwa kuna mtu anahitaji unga.
Kijana huyo anafungua begi dogo alilokuwa amebeba ubavuni na kutoa mfuko aliojaza kete. Ninatumia nafasi hiyo kupiga picha kwa usiri wakati kijana huyo akionyesha.
Baada ya hapo, Mashikolo anarudi kuketi nilipokuwa nimekaa na kumwita kijana mwingine anayeonekana teja.
“Unga unapatikana wa shilingi ngapi hapa?” anamuuliza.
“Hapa unapatikana wa kupima kuanzia Sh2,000 lakini Feri upo wa bei ya jumla ambao unauzwa kwa kidonge,” anajibiwa na kijana huyo.
“Kidonge kimoja cha unga wa cocaine kinauzwa Sh4,000 hadi Sh6,000 lakini maeneo mengine kinauzwa hadi Sh10,000.”
Baada ya maelezo hayo, Mashikolo anamuomba yule kijana amletee unga wa Sh2,000 ili aone kipimo chake. Kijana huyo anaondoka na kuelekea upande wa mabanda na baada ya nusu saa anarejea tena akiwa na kijana mwingine.
Anakuja na unga ambao umewekwa kwenye kikaratasi cha rangi ya bluu na nyeupe. Ni mfano wa mchanga. Kisha anamwambia teja huyo achukue akatumie mwenyewe.Teja anatabasamu na kuondoka.
Kambi za wavuvi wa samaki Feri
Baada ya kuona biashara hiyo, tukaondoka kuelekea Feri. Tulifika eneo ambalo wavuvi hushushia samaki wao. Kulikuwa na watu takribani 200. Hapa kumetawaliwa na harufu ya uozo pamoja na bangi.
Mashikolo anasema eneo hili ndilo maarufu kwa uingizaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwa bei ya jumla na rejereja. Eneo hilo lina vibanda kadhaa vilivyojengwa kwa miti myembamba na kuezekwa kwa maturubai yaliyochakaa kiasi kwamba watu waliokuwa ndani na shughuli walizofanya zilionekana.
Wapo waliokuwa wanakula chakula na wengine wakivuta bangi na sigara. “Watu unaowaona hapa wengi si wema. Hapa ukitaka dawa za kulevya aina yoyote unapata,”anasema Mashikolo.“Si unaona huko ndani kwenye mabanda, biashara inaendelea na unaona watu wanavuta bangi hadharani. Eeh! Unamuona yule baba mrefu aliyevaa shati la drafti na miwani?” ananiuliza.
“Yule ni askari mpelelezi, anaona watu wanavuta lakini hana cha kufanya, anawaangalia tu.”
Haya yote yanafanyika mita chache kutoka jengo la Ikulu. Biashara ya mihadarati inafanyika waziwazi. Tulitembea kama hatua kumi kutoka eneo la wavuvi na kusimama, kisha Mashikolo akanieleza jinsi meli kubwa zinavyoingiza dawa hizo.
“Si unaona zile meli kule, hizo ndizo hutumika kuingiza dawa za kulevya na kuzifaulisha kwenye boti ndogo za wavuvi. Wavuvi wakishusha samaki wanashusha na dawa za kulevya. Kwa hiyo hapa ni kama kitovu cha madawa. We mwenyewe unawaona watu wa hapa walivyo,” anasema.
Sianga aelezea mikakati yake
Maelezo ya Mashikolo yalisababisha nifanye jitihada za kukutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rodgers Sianga kujua taasisi yake inafahamu vipi biashara hiyo.
Na maelezo yake yaliniacha mdomo wazi.
Kamishna Sianga anasema vita dhidi ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya ni ngumu na hatari kuliko wengi wanavyoamini, na wakati mwingine wamejikuta wakihatarisha maisha yao.
“Tunapambana. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunadhibiti na kuua kabisa mtandao wa waingizaji na wauzaji wa dawa za kulevya, na katika hili tunapata mafanikio makubwa,” anasema.
“Mpaka sasa tumewakamata mapapa 15 wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo hapa nchini. Si kwamba tumefanikiwa kumaliza tatizo, lakini jamii inatakiwa kujua biashara hii ina mtandao mkubwa ni wa watu wenye pesa nyingi. Tumekamata hao 15 lakini kuna kundi jingine tena limeibuka.
“Yaani iko hivi, mkiwakamata hawa unaibuka mtandao mwingine. Kwa hiyo si kazi ndogo. Tunapambana sana kiasi kwamba tunatishiwa kuuawa.” Anasema wanaoendesha biashara hiyo ni watu wenye jeuri ya pesa.
“Nakumbuka wakati tunaenda kumkamata mmoja wa kigogo wa unga (alimtaja jina), alitaka kuonyesha jeuri ya pesa. Tulipofika kwake akawaambia vijana wake ‘wana njaa tu hao waulize wanataka shilingi ngapi?’,” anasema.
“Kinachoshangaza zaidi watu hawa wana mtandao ulioingia hadi ndani ya Serikali kwa maana kwamba wapo watu ndani ya Serikali wanafahamu shughuli zao na wanawalinda. Wengine ni wafadhili wakubwa ndani ya makanisa na kwenye jamii, wapo ambao ukitokea misiba kwenye jamii zao wao wanaubeba kwa kila kitu mpaka mazishi.
“Nilipomkamata muuzaji mmoja (anamtaja) baadhi ya viongozi wa dini na vigogo wa Serikali walianza kunipigia simu na wengine kunifuata ofisini wakilalamika kwa nini nimemkamata mfadhili wao na wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai kuwa tumemuonea.”
Sianga anasema taarifa walizonazo muhusika mmoja wa dawa hizo ambaye alimtaja jina, alikuwa ni mfadhili mkubwa wa ofisi moja ya Serikali. Anasema mtu huyo alikuwa akigharimia matengenezo ya magari ya ofisi hiyo na kusomesha mpaka watoto wa watumishi wa Serikali. Anasema wakati mwingine hugharamia sherehe za harusi za watoto wa vigogo wanaomlinda na hata kuwalipia mahari.
Anasema kiongozi mmoja wa ofisi ya Serikali, ambaye alimtaja jina, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakimlinda (muuzaji huyo) ili asikamatwe, hata juhudi za kumkamata zilipofanyika, alikuwa anavujisha siri.
Anasema muuzaji huyo wa dawa za kulevya, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha gerezani, anaishi gerezani kama mfalme.
“Tunapata taarifa kutoka gerezani kuwa anahudumiwa vizuri na inavyosemekana huenda wakati mwingine halali hata gerezani,” anasema.
Kamishna wa masuala ya sheria wa mamlaka hiyo, Edwin Kakolaki anasema yupo mtu aliyefungwa kwa biashara ya madawa lakini anaishi gerezani kama mfalme na anaendesha biashara yake kama kawaida.
“Mbaya zaidi akiwa gerezani alinunua nyumba na watu wakachukuliwa kwenda kukaa katika nyumba ile kwa kazi moja tu ya kumpikia chakula.
Anasema nyumba hiyo hutumika kupikia chakula asubuhi na mchana kwa ajili ya mfungwa huyo wa dawa za kulevya na wakati anapoumwa, mkuu wa gereza huagiza apelekwe hospitali ambako pia huhonga ili alazwe hata wiki tatu.
Itaendelea kesho








Previous
Next Post »