Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza sababu ya kumteua Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro huku akimhimiza akachape kazi.
Rais Magufuli ametaja sababu hiyo wakati wa hafla ya kumwapisha Mghwira iliyofanyika leo, Jumanne jijini hapa na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Mimi huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu na wewe nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia wananchi, nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro,”amesema Rais Magufuli na kuongeza;
“Wapo watu watakaokusema na wengine watakuonea wivu, wewe kachape kazi.”
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa atapata ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na asikubali kuyumbishwa na mtu yeyote katika majukumu yake.
Mghwira amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Saidi Meck Sadiki aliyekuwa mkuu wa mkoa huo.
Kwa upande, Mghwira amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na amemuahidi kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kujenga Taifa.
“Ninasema hii ni heshima kwa Taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na minong’ono mingi sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani, mimi sio mpinzani wa maendeleo,” amesema Mghwira.
Sign up here with your email