IGP SIRRO ASUBIRIWA NA WAZEE RUFIJI , KIBITI - Rhevan Media

IGP SIRRO ASUBIRIWA NA WAZEE RUFIJI , KIBITI

Wazee mbalimbali kutoka maeneo tofauti tofauti
Wazee mbalimbali kutoka maeneo tofauti tofauti katika wilaya za Kibiti na Rufiji wakimsubiri IGP Sirro kuzungumza nae katika ukumbi wa mikutano kwenye shule ya sekondari Kibiti.Picha na Azory Gwanda 

Rufiji. Wazee mbalimbali kutoka maeneo tofauti tofauti katika wilaya za Kibiti na Rufiji wakimsubiri  Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP), Simon Sirro kuzungumza nao katika ukumbi wa mikutano kwenye Shule ya Sekondari Kibiti.
Sirro anafanya ziara yake ya kwanza katika wilaya hizo tangu alipoteuliwa kuwa IGP ili kuzungumza na wazee hao na wakazi wa maeneo hayo kutokana na mauaji yanayoendelea.
Watu zaidi ya 30 wameuawa na watu wasiojulikana katika wilaya hizo jambo lililosababisha Serikali kuifanya kanda maalum ili kudhibiti mauaji.
Baadhi ya wazee waliozungumza na gazeti hili hivi karibuni walitaka Sirro kufika na kuzungumza na wazee kuhusu mauaji yanayoendelea.
Mkazi mmoja wa Kibiti aliyejitambulisha kwa jina la Alhaji Msumi alisema IGP Sirro anapaswa kufika katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kisha kufanya mazungumzo na wazee.
Alisema akikaa na wazee waliopo katika vijiji vya Bungu, Kibiti na Ikwiriri ataweza kubaini ni nini sababu ya mauaji hayo na wahusika wanaoendesha mauaji hayo na suluhisho lake.
Alisema kwa sasa Jeshi la Polisi linapaswa kuongeza askari wa upelelezi na kuruhusu shughuli za nyingine za biashara kuendelea, huku akikazia pikipiki kuendelea kutotumika kuanzia saa 12 jioni kama agizo lilivyotolewa.
Msumi alisema wananchi wapo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola vitakavyokuja ili kuwabaini wahusika wa mauaji hayo.
Alisema awali kikosi kilichokuwepo katika miji hiyo kilikosa ushirikiano wa dhati toka kwa wananchi kwa kuwa Polisi walioletwa walikuwa wakiwapiga wananchi ovyo, hali iliyosababisha wananchi wengi kutotoa ushirikiano wa dhati kwa jeshi hilo.
Msumi alisema anafahamu uwezo wa IGP Sirro katika utatuzi na ufumbuzi wa migogoro mingi iliyosimamiwa naye akiwa katika nyadhifa mbalimbali alizozipitia, ikiwa ni pamoja na namna alivyofanikiwa kuutatua mgogoro wa vurugu za mwaka 2012 uliotokea Ikwiriri kati ya wenyeji na wageni hususani wa jamii ya wafugaji.
Mzee  mwingine wa Ikwiriri ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema uzoefu wa Sirro katika utulizaji na utatuzi wa matatizo utafanikisha kuwabaini watu au kikundi  wanaoendesha mauaji katika wilaya hizo.








Previous
Next Post »