DARUSO YAWANYOOSHEA KIDOLE WANAOPINGA JITIHADA ZA JPM - Rhevan Media

DARUSO YAWANYOOSHEA KIDOLE WANAOPINGA JITIHADA ZA JPM

 Uongozi wa Selikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) umesema wanasiasa wanaopinga jitihada za rais katika masuala ya maendeleo hususan suala la madini waogopwe kama ukoma.
Akizungumza  na waandishi wa habari leo (Ijumaa) Rais wa  Daruso, John Jeremia amesema ni muhimu kwa Watanzania kuungana na kuacha kuleta siasa katika mambo yaliyo na tija kwa Taifa.
"Sisi kama wasomi tupo bega kwa bega na rais kwa sababu mambo anayoyafanya hayahusiani na uchama na yamejikita kwa maslahi mapana ya taifa," amesema.
Amesema jitihada hizo hazipaswi kubezwa kwakuwa taifa limepoteza fedha nyingi ambazo zingeweza kusaidia kila mwanafunzi kupata kitabu chake kwa kila somo jambo ambalo lingesaidia katika uboreshaji elimu nchini.

"Kwa mwaka huu wa fedha ya mkopo kwa ajili ya wanafunzi ni Sh483bilioni tu kiasi ambacho hakitoshelezi pengine fedha hiyo ingeelekezwa japo kiasi katika elimu migomo isingekuwepo," amesema.
Amesema ni jambo la kusikitisha mno kuwa wapo wanasiasa na wasomi wanaopinga hatua hii dhidi ya ukombozi wa uchumi wa taifa ijapokuwa wengi wao wamesoma chuo hicho mama.
"Hatujivunii wanasiasa wanaopinga jitihada za kulikomboa taifa na wameitia aibu taasisi yetu, hawakustahili kusoma kwa kodi za Watanzania na kupata digrii katika chuo chetu," amesema.
Kwa upande wake Makamu wa rais wa chuo hicho, Anastazia Anthony amesema wanafunzi wote wanaotarajia kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano bora na kutanguliza maslahi ya taifa mbele.







Previous
Next Post »