Dodoma. Haikuwa lelemama kuipitisha bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Wapo wabunge waliojichanganya, huku mzozo wa muda mfupi ukimtoa ukumbini Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara.
Juzi jioni baada ya mjadala wa zaidi ya wiki moja, jumla ya wabunge 355 walishiriki kuipigia kura bajeti ya Sh31.7 trilioni. Wabunge 260 waliikubali bajeti hiyo lakini wengine 95 waliikataa. Idadi ya wabunge wote kikatiba ni 393.
Bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika ilipigiwa kura zote za ndiyo na wabunge 251, wabunge wa upinzani hawakuwamo ukumbini.
Kanuni zinaelekeza akidi ya kikao cha Bunge kuendelea ni nusu ya wabunge na ili Bajeti hiyo ipitishwe inatakiwa kupigiwa kura ya ndiyo na nusu ya akidi ya wabunge.
Wabunge wa upinzani wanaoipigia kura ya ndiyo bajeti ni wale waliotofautiana na wenzao.
Hata hivyo, bajeti iliyopitishwa juzi ilitawaliwa na vituko ikiwamo baadhi ya wapinzani kuikubali lakini hapo hapo wakabadili msimamo.
Juzi asubuhi, Spika alitahadharisha kwamba kutoipitisha bajeti inamaanisha kulivunja Bunge hilo hivyo, kurudiwa kwa uchaguzi ili kuwapata wawakilishi wapya.
“Ikitokea lisilotarajiwa kwamba bajeti hii imekataliwa basi maana yake hata sisi wenyewe sio wabunge na tutatakiwa kwenda kwenye uchaguzi. Wale wenzetu wanaopenda kutoka nje, mmoja mmoja hata mkiwa 10 basi mnatoka taratiiibu. Ingawa sitarajii ila likitokea sitashangaa,” alisema Ndugai.
Utabiri huo ulitimia, japo kwa namna nyingine. Hakuna aliyetoka kwa hiyari yake bali kwa amri ya Spika huyo. Ingawa ilikuwa ni baada ya kura kupigwa, Ndugai aliamuru Waitara atoke nje kwa hiyari yake kabla askari wa Bunge hawajamuondoa kwa mabavu.
Kilichomuondoa Waitara ni kuomba kutoa taarifa kwenye kipindi ambacho Spika alisema ni cha miongozo.
Kabla Waitara hajaondolewa, Spika alitoa ufafanuzi kwa muongozo ulioombwa na Mbunge wa Mbeya Mjini(Chadema), Joseph Mbilinyi aliyetaka kufahamu inakuwaje wapinzani waliopiga kura ya hapana waonekane hawastahili kupelekewa miradi ya maendeleo ilhali fedha ni za wananchi.
Kwenye ufafanuzi wake, Ndugai alisema mbunge anaposema ndiyo huo ni msimamo wa anaowawakilisha na akikataa maana yake wamesema hapana. Alishangaa kuwapo kwa wananchi wasiotaka kero zao zitatuliwe kwenye maeneo yao.
“Nawashangaa mawaziri, mtu anakataa bajeti machoni kwenu lakini kesho anakuja anasema hiki na hiki hakijatekelezwa. Najua kuna watu wamelazimishwa kusema hapana na si kwa ridhaa yao. Ukiona mtu anasema hapana kwa bajeti ambayo ina mshahara wake mwenyewe basi unamsamehe bure,” alisema.
Upigaji kura
Wabunge wote wa chama tawala walisema ndiyo, lakini ilikuwa tofauti kwa wapinzani wanaunganishwa chini ya mwamvuli wa Ukawa.
Wabunge wawili walijichanganya; badala ya kusema hapana kwa mara ya kwanza, walisema ndiyo ingawa marekebisho ya kura zao yalifanyika baadaye.
Alianza Mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga aliyepiga kimakosa kura yake. Alisema ‘ndiyo’ wakati akimaanisha ‘hapana.’
Baada ya kuona anashangiliwa na CCM alishituka akapiga kelele: “Hapana…hapana...hapanaaaa.” kwa busara zake, Spika aliagiza kura hiyo irudiwe na Kiwanga akasema ‘hapana’ ya uhakika.
Kilichomtokea Kiwanga kilijirudia kwa Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mwanza (Chadema), Suzan Masele. Alisema ‘ndiyo’ kisha akaifuta.
Wabunge wawili wa CUF wanaounga mkono upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) na Magdalena Sakaya (Kaliua), walipiga kura ya ndiyo na kushangiliwa na wabunge wa CCM huku wakiitwa wazalendo.
Kulikuwa na kelele pia baada ya kuitwa kwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kutoka mkoani Kagera, Halima Bulembo. Kelele hizo zilitokea baada ya Halima kuitwa muda mfupi baada ya baba yake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo kupiga kura yake.
Sign up here with your email