ALICHOKISEMA KAFULILA BAADA YA SERIKALI MKOANI KILIMANJARO KUHARIBU SHAMBA LA MBOWE - Rhevan Media

ALICHOKISEMA KAFULILA BAADA YA SERIKALI MKOANI KILIMANJARO KUHARIBU SHAMBA LA MBOWE

Tokeo la picha la kafulila bungeni
ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amelaani hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa kutumia mamlaka yake kuvamia na kuharibu shamba la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Juzi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya walivamia shamba la Mbowe nyumbani kwake Machame na kuharibu miundombinu, mali, mboga na mimea kadhaa.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kafulila alisema amesoma na kusikia kuwa Mkuu huyo alitumia mamlaka yake kufanya kitendo hicho, jambo ambalo aliliita ni laana ya hali ya juu.

“Nimesoma na kusikia kuwa Mkuu wa Wilaya ametumia mamlaka yake kuvamia na kuharibu shamba la Mwenyekiti wa Chadema ambalo ni uwekezaji wa kilimo cha mboga kwa soko la ndani na nje ya nchi,” alisema.

Alisema kitendo hicho ni cha kushangaza, kwa kuwa shamba hilo lina thamani ya mamilioni ya fedha, lakini mtu anatokea na kuharibu miundombinu kwa kuwa ni kiongozi tena bila sababu za msingi jambo ambalo halileti picha nzuri kwa jamii.

“Huu ni uamuzi unaoweza kufanywa na Serikali za kishenzi kama Somalia au Sudani na Burundi. Nasita kuamini kama huko ndiko Rais John Magufuli anataka kutupeleka,” alisema na kuongeza:

“Naamini atachukua hatua kali dhidi ya DC huyu, kwani ni doa lenye viashiria vya chuki za kisiasa kwa kiwango cha unyama, chuki ambayo hakika sidhani kama inaweza kuwa maelekezo ya kiongozi anayemtaja Mungu na kuomba maombi siku zote.”
Previous
Next Post »