WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATEMBELE MASHINE MPYA ZA KUSAGIA TAKATAKA ZA HOSPITALI - Rhevan Media

WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR ATEMBELE MASHINE MPYA ZA KUSAGIA TAKATAKA ZA HOSPITALI

unnamed

Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akipata maelezo ya mashine mpya ya kusagia taka za hospitali kwa Mtaalamu wa mashine hizo kutoka Kenya Benard Abere.
         
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amesema tatizo la kuharibika kwa mashine ya kusagia taka katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja siku za karibuni kulipelekea kurundikana kwa taka na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Amesema baadhi ya wafanyakazi wakorofi wa Hospitali hiyo walitumia kasoro hiyo kuzitupa taka kwenye ufukwe wa bahari, nyuma ya Hospitali, ambapo ni kosa kwa mujibu wa sheria na kanuni za afya na uhifadhi wa mazingira.
Waziri Mahmoud ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kutembelea mashine ya kusagia taka zinazozalishwa katika Hospitali hiyo ambayo hivi sasa imefanyiwa matengenezo na ipo tayari kufanyakazi na kuondosha kero hilo.
Amesema wafanyakazi saba waliobainika kufanya kosa la kutupa taka sehemu ya ufukwe wamechukuliwa hatua za nidhamu na kuuagiza uongozi wa Hospitali ya Mnazimmoja kutomvumilia mfanyakazi atakaekiuka kanuni za afya.
Hata hivyo Waziri wa Afya amekiri kuwa uzalishaji wa taka katika Hospitali ya Mnazimmoja umekuwa mkubwa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa baada ya kutanuliwa na kufikia daraja la kuwa Hospitali ya rufaa.
Ameyashauri Makampuni yanayohitaji taka kwa ajili ya kuzisarifu na kuzigeuza kwa ajili ya matumizi mengine waonane na uongozi wa Hospitali kwani sehemu kubwa ya taka hizo zinaweza kutumika kwa shughuli nyengine.
Amesema hivi sasa uongozi wa Hospitali ya Mnazimmoja umeandaa utaratibu mzuri wa kukusanya taka ambapo za aina moja zinatiwa katika pipa moja na mapipa hayo yamewekwa katika wodi ili kuondosha usumbufu kwa wafanyakazi, wagonjwa na watu wanaofika kwa shughuli mbali mbali.
“Nataka wananchi wawe waangalifu wakati wa kuhifadhi taka kwani  kila pipa linatiwa taka maalumu na hakuna kuchanganya taka zote katika pipa moja,” alisisitiza Waziri Mahmoud. 
Amewataka wafanyakazi wa Hospitali kusimamia na kuwaelimisha wananchi matumizi ya mapipa hayo ili kila pipa liingizwe taka zinazostahiki ili kuondosha usumbufu wakati wa zoezi la kuzisaga.
Mtaalamu wa mashine ya kusagia taka kutoka Kenya Benard Abere amemueleza Waziri wa Afya kwamba kazi ya kuifanyia matengenezo mashine hiyo imekamilika na katika kipindi cha wiki moja mkusanyiko wa taka utaondoka       
Previous
Next Post »