UDHIBITI WASAFIRISHA MKAA KWA PIKIPIKI , BAISKELI UTAONGEZA MAPATO YA SERIKALI - Rhevan Media

UDHIBITI WASAFIRISHA MKAA KWA PIKIPIKI , BAISKELI UTAONGEZA MAPATO YA SERIKALI

Tokeo la picha la PIKIPIKI  MKAAWafanyabiashara wa mkaa wakisubiri wateja katika soko la Songasi, Mbande jijini Dar es Salaam.Picha ya maktaba 

Wakati zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wakielezwa kutumia mkaa kama chanzo kikuu cha nishati, huku zaidi ya asilimia 50 ukitumika jijini Dar es Salaam, msako wa kuwadhibiti wanaousafirisha kwa pikipiki au baiskeli umeanzishwa.
Taarifa zinaonyesha mkaa husababisha upotevu wa wastani wa hekta 372,000 za misitu kila mwaka. Uvunaji huo hupoteza walau asilimia 1.1 ya eneo lote la misitu nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack anasema tani milioni 2.3 za mkaa zilitumika mwaka 2012 na kwamba, kiwango hicho kitakuwa maradufu ifikapo mwaka 2030.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umekuwa ukibainisha namna taifa linavyopata hasara kutokana na uvunaji huo sambamba na usafirishaji mazao ya misitu kwa kutumia baiskeli na pikipiki, hivyo kukwepa tozo na kodi zinazostahili.
Kukabiliana na changamoto hiyo, wakala umeanzisha msako dhidi ya vyombo hivyo vya usafirishaji. Aprili, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Glory Mziray alisema sheria na kanuni za misitu zinapiga marufuku mazao ya misitu kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na baiskeli.
Kwa mujibu wa mwongozo wa uvunaji endelevu wa mazao ya misitu ya asili wa mwaka 2015, vyombo vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao hayo ni vyenye magurudumu manne.
Msako wa kuhakikisha Serikali inapata mapato yake inayostahili ulioanzishwa na wakala huo, umefanikisha kuzinasa pikipiki 46 na baiskeli 30 jijini Dar es Salaam zikisafirisha mkaa kupeleka kwenye maeneo mbalimbali.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Profesa Romanus Ishengoma anasema ingawa Dar es Salaam inaongoza kwa kuunganishwa na umeme na gesi ya nyumbani, ndiyo yenye watumiaji wengi wa mkaa.
“Zaidi ya asilimia 50 ya mkaa unaochomwa nchini, unasafirishwa na kutumiwa na wakazi wa Dar es Salaam,” anasema Profesa Ishengoma wakati akichangia kwenye mkutano wa wadau wa mkaa jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mawasiliano wa wakala huo, Tulizo Kilaga anasema kukamatwa kwa vyombo hivyo ni matokeo ya ushirikiano baina yao na Kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
“Ushirikiano huu umesaidia kukabiliana na tatizo hilo, kwa sasa tutahakikisha njia zote wanazotumia kufanikisha lengo lao ovu tunadhibiti ipasavyo,” anasema ofisa huyo.
Kilaga anasema pikipiki na baiskeli hizo zinashikiliwa kwa kosa la kusafirisha mazao ya misitu kinyume cha sheria kwa kuwa mazao hayo yaliyopatikana isivyo halali, jambo ambalo linaikosesha mapato Serikali na ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.
Anasema vyombo hivyo vilikamatwa kwa nyakati tofauti katika barabara kuu zinazoingia jijini Dar es Salaam hasa zinazotokea Bagamoyo, Kilwa, Kisarawe na Morogoro.
Kwa mujibu wa sheria zinazozuia uharibifu wa mazao ya misitu na usafirishaji wake, kila pikipiki itatozwa faini ya Sh500,000 huku baiskeli zikitozwa faini isiyopungua Sh50,000.
“Sheria ya Misitu inaeleza wazi kuwa mtu yeyote anayesafirisha mazao ya misitu yaliyopatikana kinyume cha sheria akikutwa na hatia atatakiwa kulipa faini isiyozidi Sh1 milioni au mara tatu ya thamani ya mazao ya misitu yaliyokamatwa, au kifungo kisichozidi miaka saba au adhabu zote kwa pamoja,” anasema Kilaga.
Anaongeza kwa wiki mbili za zoezi hilo jijini Dar es Dar es Salaam, zaidi ya Sh11.167 milioni zimepatikana kutokana na faini iliyotozwa kwenye magari yaliyokutwa na mazao ya misitu kinyume na sheria ya misitu na moja lipo katika ofisi ya meneja TFS wilayani Bagamoyo kwa hatua zaidi.
Kilaga anasema pikipiki na baiskeli zilizokamatwa zimehifadhiwa katika ofisi ya Meneja Misitu Wilaya ya Temeke, Bagamoyo na Kibaha huku magunia 451 ya mkaa ambayo yanakadiriwa kuwa na thamani ya takriban Sh10 milioni yakishushwa kutoka katika pikipiki na magari yaliyokaguliwa.
Anasema mkaa uliokamatwa umehifadhiwa katika ofisi ya Meneja Misitu wa Wilaya ya Mkurunga, Kituo cha Ukaguzi Vikindu na ofisi ya Meneja Misitu Wilaya ya Ilala.
Kwa mujibu wa ofisa huyo ukaguzi wa udhibiti wa vyombo vinavyosafirisha mazao ya msitu kinyume na sheria, hususan baiskeli na pikipiki nchini ulianza Aprili 14 na unafanyika usiku na mchana na kwamba, ni endelevu.
Wananchi
Baadhi ya wananchi wanaipongeza Serikali kwa kuwabana wenye baiskeli na pikipiki kutojihusisha na biashara hiyo, hivyo kutumika kama chanzo au kichocheo cha uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti.
“Wakati naipongeza Serikali kuwabana hawa watu wenye hivi vyombo hawapaswi kuvitumia kwa kuwa ni vyepesi viwapo barabarani, ni rahisi kupata ajali vikizidiwa na uzito,” anasema Luksai Losway, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam na kuongeza:
“Huwezi kulinganisha gari na pikipiki, mwenye pikipiki au baiskeli upepo tu unaweza kumuondoa barabarani akaangukia mtaroni.”
Mkazi wa Temeke Stereo, Masoud Luftahi anahoji kama sheria ipo inayodhibiti vyombo hivyo vya usafiri kubeba mizigo hiyo, kwa nini ilikuwa haitekelezwi na kuwataka wasimamizi wake kuhakikisha inafuatwa.
“Itakuwa jambo la kushangaza kama kwa wiki mbili tu wamekamata pikipiki na baiskeli nyingi hivyo, halafu wasiendeleze moto huo. Pia, nawaomba waingie zaidi vijijini,” anasema.
Anaitaka Serikali kutunga sheria kali zaidi kudhibiti usafirishaji holela wa mazao ya misitu, ikiwamo kuni ambazo matumizi yake yapo juu na zinasafishwa kwa urahisi na watu wenye pikipiki pamoja na baiskeli.







Previous
Next Post »