TANESCO WAKATA UMEME KAMBI YA JWTZ , MAGEREZA NA POLISI ... OFISI YA MKUU WA MKOA NAYO NUSURA IKATIWE - Rhevan Media

TANESCO WAKATA UMEME KAMBI YA JWTZ , MAGEREZA NA POLISI ... OFISI YA MKUU WA MKOA NAYO NUSURA IKATIWE

Agizo la Rais Dk. John Magufuli la kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuzikatia umeme taasisi za Serikali zinazodaiwa jumla ya Sh bilioni 8.6 limeanza kufanya kazi mkoani  Arusha.

Ofisi zilizoanza kuonja machungu ya kukosa umeme kuanzia jana hadi zitakapolipa madeni ni Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Oljoro, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Magereza, Hospitali za Serikali na Taasisi za Maji.

Nyingine zilizokatiwa umeme ni Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha ikiwamo Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha na Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha.

Wakati ofisi hizo zikikosa umeme, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilinusurika baada ya kuanza kulipia deni lake la Sh milioni sita 6 kwa awamu.

Akithibitisha kufanyika kwa operesheni hiyo iliyotajwa kuwa endelevu kwa ofisi hizo mkoa mzima, Ofisa Uhusiano wa Tanesco mkoani hapa, Saidy Mremi, alisema inalenga kukusanya madeni yote ya miaka iliyopita.

“Tunatekeleza agizo la Rais Magufuli, hatutaziacha salama ofisi zote zinazodaiwa. Tunafanya hivi ili kuiwezesha ijiendeshe pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” alisema.

Mremi alisema operesheni hiyo iliyoongozwa na Meneja wa Tanesco Kanda, Stella Hizza na Meneja wa Mkoa, Gasper Msigwa, ilikata umeme katika vituo vya polisi vilivyopo mjini hapa.

Pia alivitaja vituo vya polisi vingine vilivyokatiwa umeme kuwa ni vituo vya Polisi vya Unga Limited, Ngarenaro, Sakina na Ngaramtoni.

“Vituo vingine ni Sekei, Fire, Kijenge, Chekereni, Olorien na Mbauda. Na vituo vingine vya jeshi likiwamo Duka la Jeshi lililoko JKT Oljoro na Njiro Nane Nane. Hii ni operesheni endelevu itakayowezesha shirika kujiendesha,” alisema.

Akielezezea kuhusu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alisema ofisi hiyo imeweza kutoa ushirikiano wa hali juu katika kulipia deni lao.

“Hawa tulikuwa tunawadai shilingi milioni sita hadi sasa wameweza kulipia zaidi ya asilimia 80 ya deni lao, wametupa ushirikiano wa hali ya juu na wameahidi kuendelea kulipa ili kumaliza deni lao,” alisema.

Mremi alisema madeni hayo ni ya miaka ya nyuma na yalitokana na taasisisi hizo kuyalimbikiza kisha yakahamia mwaka mwingine.

Aliyataja madeni ambayo taasisi hizo zinadaiwa (kwenye mabano) kuwa JWTZ (Sh milioni 538), JKT (Sh milioni 57), Jeshi la Polisi (Sh milioni 490), Jeshi la Magereza (Sh Milioni 271), hospitali tofauti za Serikali (Sh milioni 58) na taasisi nyingine ikiwamo za maji (Sh milioni 106).

“Taasisi hizi za Serikali kwa ujumla wake zinadaiwa shilingi bilioni 8.6 sawa na asilimia 28 na asilimia 72 inayobakia ipo kwa taasisi, mashirika na watu binafsi,” alisema.

Kabla ya kufikia hatua hiyo ya kuzikatia umeme taasisi hizo pamoja na wateja wengine, alisema huwa wanatoa notisi kwa wateja wake ikiwamo kutangaza matangazo katika vyombo vya habari.
Previous
Next Post »