SIRI INAYOWAKIMBIZA WAGOMBEA CCM YATAJWA - Rhevan Media

SIRI INAYOWAKIMBIZA WAGOMBEA CCM YATAJWA

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mikoa
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mikoa mbalimbali wakishangilia walipohudhuria mkutano maalumu kwa ajili ya kupitisha mabadiliko ya katiba na kanuni za chama hicho mjini Dodoma, Machi 12, mwaka huu. Picha na Maktaba 

Dar es Salaam. Uchaguzi wa viongozi wa CCM katika ngazi ya shina na matawi umekumbwa na tatizo la wanachama kutojitokeza kugombea, hali ambayo baadhi ya wadau wamesema imesababishwa na nafasi hizo kutokuwa na umuhimu na kutokuwa na posho.
CCM, ambayo hufanya chaguzi zake kila baada ya miaka mitano, imeanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wapya kutokea ngazi ya shina, lakini mabadiliko ya katiba yaliyofanywa hivi karibuni na sera za uongozi wa sasa yameufanya uchaguzi huo kukumbwa na changamoto, hasa ya wanachama kugombea nafasi za ngazi ya chini.
Awali ngazi ya kwanza ilikuwa ya mjumbe wa nyumba kumi, lakini sasa imekuwa shina ambalo kila moja linatakiwa kuwa na watu angalau 50.
Pia, sera ya sasa ya uongozi inataka mwanachama kuwa na nafasi moja ya kiutendaji badala ya kofia mbili.
Licha ya mchakato wa uchukuaji wa fomu kuanza wiki kadhaa katika ngazi ya shina na kata, ni wanachama wachache waliojitokeza kiasi cha kuwafanya baadhi ya viongozi kuwafuata watu wanaoamini kuwa wanafaa na kuwashawishi kujitokeza kugombea.
Katika Kata ya Kimanga Darajani wilayani Ilala, viongozi wa CCM walionekana wakipita nyumba kwa nyumba kuwalazimisha vijana wachukue fomu.
Habari kutoka katika kata hiyo zinaeleza kuwa licha ya fomu kuanza kutolewa tangu Januari, hadi Aprili 30 hakukuwa na wanachama waliojitokeza kuwania nafasi ya katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM na mwenyekiti wa kata wa Jumuiya ya Wazazi.
Hali hiyo iliwalazimu viongozi hao kupita nyumba kwa nyumba kuwaomba vijana kuchukua fomu hata kama hawana sifa.
“Walitulazimisha kujaza fomu za uongozi wakati sisi si wanachama. Tuliambiwa tutakatiwa kadi za uanachama hapohapo na mambo mengine watayatatua wenyewe huko,” alisema mkazi mmoja.
Kwa mujibu wa chama hicho, mtu mwenye sifa ya kuwania uongozi ni lazima awe mwanachama hai, awe amedumu kwa angalau kwa miaka mitano, anayejua kusoma na kuandika, anayekubalika kwenye jamii na anayeshiriki kikamilifu katika shughuli za kichama.
Kuhusu kusuasusa kwa uchukuaji wa fomu, kaimu katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka alisema jumuiya yake haijaliona tatizo hilo kwa sababu hawajapata malalamiko.
Alisema uchukuaji fomu unaendelea na iwapo wataona hakuna maendeleo ya kuridhisha, ndipo watakapokaa kujadili.
Pia alizungumzia masuala ya rushwa na makundi ambayo yalielezwa kuwa moja ya sababu za kusuasua kwa uchukuaji huo wa fomu na kusema katika hatua za awali waliliona hilo na kutoa maelekezo na onyo kali kwa yeyote atakayethubutu kufanya usumbufu wa aina yoyote kwa wanaohitaji fomu za kugombea uongozi.
Hata hivyo, alisema hawajapata malalamiko ya aina yoyote wala kusikia harufu ya rushwa.
Alisema katika baadhi ya mikoa ikiwamo Katavi, asilimia 40 ya waliochukua fomu ni vijana na mkoani Rukwa ni asilimia 45.
“Hilo kwetu tunalichukulia kama mafanikio. Vijana kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali, huku wakipata huduma hiyo bila vikwazo vyovyote (ni jambo zuri),” alisema.
Akizungumzia suala la fomu, diwani wa Manchali wilayani Chamwino, Mary Mazengo alisema wanachama wanagoma kujitokeza kwa sababu ya kupungua kwa thamani ya nafasi ya mwenyekiti wa shina.
“Wanasema kazi nyingi kwa sasa zinafanywa na mwenyekiti wa kitongoji kwa hiyo mwenyekiti wa shina hatakuwa na kazi. Lakini hata ushirikiano hawapati kwa mwenyekiti wa kitongoji,” alisema.
“Lakini bado tunaendelea kutoa elimu kwa wanachama, uelewa pia mdogo katika ngazi ya shina, matawi.”
Diwani wa Kibuko wilayani Morogoro Vijijini, Mary Kunambi alisema wanaosusia kugombea nafasi hizo ni pamoja na makatibu wa matawi kwa madai ya kutolipwa posho za uchaguzi wa mwaka 2015.
“Wanachama wapo ila tatizo ni makatibu wanagoma kabisa, hadi wapewe posho zao. Katika kata yangu kuna mashina 75 na matawi saba. Kwa sasa uchukuaji fomu unamalizika leo (jana) kwa hiyo tunaendelea kuwashawishi,” alisema.
Diwani wa Songwe wilayani Kishapu, Abdul Ngoromole alisema ugumu wa maisha unawafanya wasite kujitokeza kugombea nafasi hizo.
“Mwanachama anaona bora ajitafutie kibarua kingine badala ya uongozi usiokuwa na posho. Pia kazi nyingi zinafanywa na wenyeviti wa vitongoji kwa hiyo thamani inakuwa imepungua. Tunaendelea kuwaelimisha,” alisema Ngoromole mwenye mashina 42 na matawi matatu katika kata yake.
Alisema changamoto nyingine ni mabadiliko ya katiba yanayosababisha baadhi ya wanachama kutojua namba ya mashina wanayotaka kugombea na wanachama wengi kukosa kadi za chama.
Hali kama hiyo imeikumba kata ya Regicheri iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambako diwani wake, John Mbusiro alisema wameshindwa kufanya uchaguzi katika zaidi ya mashina 30 na matawi manne licha ya kuwashawishi wanachama kujitokeza.
“Suala la mwitikio bado ni changamoto lakini kuna vijana wamemaliza sekondari tunajaribu kuwashawishi, isiwe kwa wazee tu,” alisema.
Diwani wa Handali, Wilaya ya Chamwino, Devota Mbogoni alisema pamoja na kuwapo kwa mwitikio wa kuomba uongozi, wanachama wengi hawakubaliani na kuvunjwa kwa mashina.
“Matawi ya karibu walikubali yaunganishwe ila ya mbali ikaonekana wanachama wengi wangekosa mawasiliano ya kichama hivyo yakaachwa, lakini tunaendelea kuwaelimisha na wanakubali,” alisema.
Hali ya uchaguzi katika kata ya Gwipirwo katika Halmashauri ya Tarime imeathiriwa na ukosefu wa kadi na posho.
Diwani wa kata hiyo, Adam Nyawambara alisema: “Mwanachama anaona bora afanye kazi zake binafsi kwa sababu hakuna malipo yoyote kwenye chama. Uchaguzi unadorora. Kata ina matawi mawili, bado hatujafanya uchaguzi ila maandalizi yanaendelea,” alisema.
Kwa Mkoa wa Mbeya nako ‘figisufigisu’ zilitawala uchaguzi huo, hususan katika Kata ya Ubaruku wilayani Mbarali, ambako kuviongozi wametuhumiwa kuweka urasimu katika uchukuaji fomu.
Akizungumza na Mwananchi, katibu wa CCM wa Kata Kata ya Ubaruku, Salvatory Malanji aliwatuhumu viongozi wa sasa kuwa wamekuwa wakitoa fomu kwa kuangalia sura.
“Si kwamba watu hawajajitokeza, hapana. Wamejitokeza wengi sana lakini shida iliyopo ni makundi. Kuna watu ambao wana lengo la kugombea nyadhifa za juu kuanzia kata na wilaya wametengeneza mtandao huku chini kwa kuwapanga watu ambao wanajua fika watawaunga mkono kwenye chaguzi zao,” alisema.
“Hili tumelibaini na tunaendelea kulishughulikia. Atakuja katibu wa Wilaya ya Mbarali kwenye kikao cha mkutano mkuu na tutajadili hili pia.”
Wakati wilayani Mbarali yakiibuka makundi hayo, katibu wa Kata ya Mbalizi Road jijini Mbeya, Adam Simbaya alisema watu wengi wamejitokeza kuchukua fomu licha ya awali kuonekana kusuasua, akisema sababu kuu ni kuhofia kigezo cha kugombea nafasi moja tu ya utendaji ndani ya chama wakati wengine walipenda kugombea ngazi ya tawi na kata.
“Kilichokuwepo hapa ni suala la kofia mbili. Mtu alikuwa anasita, eti akigombea kwenye tawi basi hataruhusiwa tena kugombea katika kata au wilaya, hivyo wengi walionekana kusita kutokana na tamaa ya kupenda madaraka sehemu mbili.”
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Kelvin Matandiko na Godfrey Kahango.     







Previous
Next Post »