SAKATA LA HOTUBA ZA WAPINZANI BUNGENI LITAFUTIWE SULUHISHO - Rhevan Media

SAKATA LA HOTUBA ZA WAPINZANI BUNGENI LITAFUTIWE SULUHISHO



Mkutano wa saba wa Bunge la 11 wa bajeti ulioanza Aprili 4 unaendelea mjini Dodoma. Tayari wabunge wamepokea taarifa ya hali ya uchumi na sasa zinajadiliwa bajeti za wizara kabla ya Waziri wa Fedha na Uchumi hajawasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Bajeti za wizara mbalimbali zimewasilishwa na kujadiliwa na Bunge, na mawaziri wamesoma hotuba zao kisha mawaziri vivuli nao kusoma bajeti mbadala kama ilivyo kawaida ya chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.
Wakati utaratibu huo wa kuwasilisha bajeti ukiendelea, kwa upande wa baraza kivuli hali haikuwa nzuri sana baada ya baadhi ya mawaziri wao kuzuiwa kusoma hotuba yote kama walivyokuwa wameziandika. Hotuba hizo zilizuiwa kutokana na kile kilichoelezwa na kiti cha Spika kuwa zima upungufu katika baadhi ya kurasa, hivyo kutakiwa kuzihariri kabla ya kuzisoma upya.
INAENDELEA UK26
INATOKA UK25
Miongoni mwa hotuba zilizozuiwa kusomwa ni ile ya Tundu Lissu wakati wa bajeti ya Katiba na Sheria; Ally Salehe (Ofisi ya Makamu wa Rais -Muungano) na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyosomwa na Joseph Mbilinyi.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wasomi waliozungumza na gazeti hili wamekuwa na maoni tofauti kuhusu utaratibu huo.
Wasomi watoa ya moyoni
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Hamad Salim anasema ingawa utaratibu uliofanyika ulifuata kanuni za Bunge, hata hivyo alihoji iwapo zinafuata misingi ya haki. Salim anasema kanuni hizo zinawanyima haki Watanzania kujua kinachoendelea kuhusu bajeti inayowasilisha na kambi ya upinzani.
Akifafanua anasema ni ingekuwa vyema vipengele vinavyogusa maisha ya Watanzania vikasomwa katika hotuba husika na siyo kuzuiwa au kuviondoa kabisa.
“Kama katika bajeti inayowasilishwa na kambi ya upinzani ina kipengele kinamtukana Rais hakifai kusomwa, lakini kukosoa taasisi za Serikali inaruhusiwa kusomwa,” anasema Salim.
Hata hivyo, anasema ni wakati mwafaka kwa kanuni zinazowanyima uhuru wananchi kusikia au kujua kilicho ndani ya hotuba mbadala za upinzani kubadilishwa au kuboreshwa.
Anasisitiza kuwa masuala yanayogusa masilahi ya wananchi ni lazima yasomwe na Watanzania wafahamu kinachoendelea isipokuwa zinazomkejeli Rais au nembo za Taifa.
Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ahmed Kiwanuka anasema kwa kuwa viongozi wa Bunge wanatumia miongozo na kanuni, huenda waliona iwapo hoja zilizozuiwa zingesomwa zingekuwa na matokeo mabaya kwa Taifa.
“Nadhani kiongozi wa Bunge alifikiri kuwa maneno yaliyomo katika hotuba za watu hao siyo mazuri kwa kikao, maana uhuru tafsiri yake siyo kuwa huru, bali ni ustaarabu na kufuata taratibu. Hata hao ambao hotuba zao zimezuiwa wakiwa katika nafasi ya wale waliowazuia hawataruhusu kila kitu kisomwe hata ambacho watadhani hakifai,” anasema.
Dk Kiwanuka anasema Bunge linawakilisha mawazo ya watu zaidi ya milioni 50, hivyo ni lazima heshima ya vikao vyake ilindwe na jambo la msingi ni wabunge pamoja na viongozi wake kuonyesha heshima.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Profesa George Shumbusho anasema kuzuiwa kwa hotuba hizo siyo jambo baya endapo kilicho ndani yake kimeandikwa kwa lugha ya kuudhi, lakini kama ni ukweli ambao baadhi ya watu hawataki kuusikia, viongozi wa Bunge watakuwa wamekosea.
“Kwa bahati mbaya sasa Bunge letu linaendeshwa kisiasa zaidi kwa masilahi ya vyama vyao, watu waliopo kule wanatanguliza masilahi binafsi mbele kuliko ya Taifa. Sifahamu kilichopo ndani ya hotuba zile, kama ni matusi hazipaswi kusomwa lakini kama ni ukweli usiopendwa kuzizua sio haki,” anasema Profesa Shumbusho.
Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke anasema kitendo cha baadhi ya wabunge kuzuiwa kuwasilisha hoja zao ni matumizi mabaya ya demokrasia.
Mbilinyi alivyozuiwa
Waziri Kivuli wa Habari, Mbilinyi maarufu kama Sugu, alijikuta matatani wakati akisoma hotuba yake baada ya kujaribu kuzungumzia sakata la kutoweka kwa kada wa Chadema, Ben Saanane.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimtaka asisome maneno yaliyo kwenye ukurasa wa 17.
Siku moja kabla ya Mbilinyi kusoma hotuba hiyo, Zungu aliagiza kuhaririwa na kuondolewa maneno yaliyokuwa kwenye ukurasa huo.
Bila kutaja maneno hayo, Zungu alisema endapo Sugu angeyasoma, kiti chake kingechukua hatua.
“Maneno yote kuanzia ukurasa wa 5-10 na ukurasa wa 35-47 yaondolewe. Yeyote anayeona hajaridhishwa na uamuzi wangu asipige kelele wala kulalamika hapa, atumie kanuni ya 5 kulalamika kwenye kamati. Tutakutana huko,” alisema Zungu.
Mara baada ya Mwakyembe kumaliza hotuba yake na kufuatiwa na ya kamati iliyosomwa na Juma Nkamia (Chemba-CCM), balaa lilianza wakati Mbilinyi alipoanza kusoma maoni ya upinzani.
Wakati akiendelea kusoma bila wabunge kupewa nakala ya hotuba hiyo, Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alisimama na kuulizia hotuba hiyo na Zungu akajibu kuwa vitabu vingeletwa baada ya muda.
Vitabu vilipoletwa, kurasa zilizotajwa zilikuwa zimeondolewa na kitabu kubaki na kurasa 29.
Mbilinyi alipotaja jina la Ben Saanane, Zungu aliingilia kati akisema hayo ndiyo maneno aliyozuia na kumtaka Sugu aruke hadi ukurasa wa 12.
Katika kurasa hizo kulikuwa na suala la kupotea kwa Saanane na viambatanisho vya kauli zake kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kupotea kwake.
Licha ya Zungu kumzuia, Mbilinyi aliendelea kusoma hata baada ya kuzimiwa kipaza sauti.
Zungu alimsihi mara nyingi mbunge huyo aache kusoma yale aliyomkataza.
“Nimeshatoa ruling (uamuzi). Usitake niende kwenye kanuni ya 74 kuhusu kudharau kiti, usitake nifanye vitu ambavyo si vizuri,” alisema Zungu.
Baada ya maelezo hayo, Mbilinyi aliondoka kwenye mimbari kwenda kukaa. Baada ya kukaa, ndipo Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu aliposimama kuomba mwongozo akisema kanuni zinazoongoza majadiliano bungeni ziko wazi, kwamba mbunge anazungumza kwanza ndipo anatakiwa kuthibitisha kama amesema uongo.
Alisema utaratibu wa makatazo kwa wapinzani wa kuwaamulia nini cha kusema ni mpya na kushauri kama ni hivyo mnadhimu wa Serikali ndiye akae kwenye kiti cha mwenyekiti.
Baada ya Lissu, alisimama Mnadhimu wa Serikali, Jenister Mhagama akisema aliyetoa mwongozo ni mwenyekiti mwenyewe na sio mnadhimu, na hivyo yeye yupo kuhakikisha kanuni zinafuatwa.
Alisema suala la Ben Sanane lilikuwa kwenye hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe na linajitokeza mara kwa mara, hivyo ni bora wakae pande mbili; upinzani na Serikali, walizungumze katika utaratibu mwingine nje ya Bunge.
Kauli ya Bulaya
Mbunge mwingine aliyesimama ni Ester Bulaya (Bunda Mjini-Chadema) aliyesema hata kama wamekuwa wakinyamaza, haina maana kwamba wapinzani hawaumizwi na mambo wanayofanyiwa bungeni.
“Tukitoka mnasema, tukikaa mnatunyanyasa. Mnataka tufanye nini? Leo mko madarakani, kesho hamko madarakani. Kwa nini mnatuchagulia cha kusema?” alihoji Bulaya.
Mambo mengine yaliyokuwa kwenye hotuba hiyo ni suala la uvamzi wa Clouds Media, shambulio la waandishi wa habari na wafuasi wa CUF-Lipumba, kukamatwa kwa waandishi kwa amri za wakuu wa wilaya, kufutwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, wizi wa kazi za wasanii na athari za kuyumba kwa uchumi kwa tasnia ya habari.

Previous
Next Post »