RC NDIKILO -AAGIZA UONGOZI ULIOPITA WA CHAURU NA MWEKEZAJI WA KICHINA KUKAMATWA - Rhevan Media

RC NDIKILO -AAGIZA UONGOZI ULIOPITA WA CHAURU NA MWEKEZAJI WA KICHINA KUKAMATWA

mwe1

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, wa katikati akizungumza jambo na uongozi wa chama cha umwagiliaji Ruvu (CHAURU), na viongozi wa wilaya, wakati alipotembelea chama hicho. (picha na Mwamvua Mwinyi) 
mwe2
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, wa kwanza kulia akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa chama cha umwagiliaji Ruvu (CHAURU) sadala Chacha mwenye kofia. (picha na Mwamvua Mwinyi) 
…………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
SERIKALI mkoani Pwani ,imetoa siku saba kwa uongozi uliopita wa Chama Cha Umwagiliaji Ruvu (CHAURU)kukamatwa na polisi pamoja na mwekezaji wa kichina ,kampuni ya M/S Guoming Tang walieingia nae mkataba feki uliogharimu dollar 35,000.
Aidha uongozi huo umetakiwa kufanya makabidhiano na uongozi mpya uliochaguliwa ndani ya wiki moja .
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi ,Evarist Ndikilo,alitoa agizo hilo,baada ya kutembelea chama hicho cha umwagiliaji ,kujionea namna wanavyoendeleza kilimo,wanavyojiendesha na changamoto zao.
Alieleza ,uongozi mpya unashindwa kutekeleza majukumu yake kwasasa kutokana na uongozi uliopita kugomea kufanya makabidhiano ya baadhi ya mali hali inayowapa wakati mgumu uongozi mpya kutekeleza majukumu yake. 
Mhandisi Ndikilo,alimuagiza kamanda wa polisi mkoani humo,kamishna msaidizi mwandamizi Onesmo Lyanga,kushughulikia agizo hilo ili hatua za kisheria na uchunguzi uchukue nafasi yake.
“Ni lazima mkataba huo upitiwe upya,na mhakikishe wote wanatiwa nguvuni na mchina wao ,ili kueleza kwanini wanang’ang’ania mali za chama na kuingia mkataba batiri kinyume na taratibu”alisisitiza.
Mhandisi Ndikilo ,alieleza kuna kitu kipo nyuma ya pazia ,ambacho kina manufaa ya matumbo ya uongozi huo kwakuwa haiwezekani washindwe kufanya makabidhiano hadi leo .
Katika hatua nyingine aliuagiza uongozi mpya kufanya tathmini ya vifaa vinavyotakiwa kwenye kinu cha mashine ya kukobolea mpunga ,ambayo haifanyikazi .
Aliwataka pia kukifanyia usafi na kuweka mazingira yake kwenye hali ya usafi tofauti na alivyokuta baada ya kutembelea kwani siyo mazingira mazuri na hayaridhishi.
Nae mwenyekiti wa ushirika huo, Sadala Chacha,alipokea maagizo waliyopewa kutoka kwa mkuu wa mkoa huyo na kusema watayasimamia .
Awali alieleza uongozi uliopita umeshindwa kuwapa ushirikiano na kufanya makabidhiano hadi sasa suala ambalo linawapa wakati mgumu.
Akizungumzia suala la mwekezaji wa kichina ,Sadala alisema hawamtambui mwekezaji huyo na hawajui mkataba wake,na wala hawajakabidhiwa mkataba huo .
Sadala alisema ,mbali ya mwekezaji huyo kuingia mkataba usiojulikana kwa wanachama pia amezuia maji yasiingie kwenye mashamba ya wanachama zaidi ya 800 hali inayokwamisha juhudi za uendelezaji kilimo.
Kutokana na mwekezaji kufunga maji,amewanyima huduma wanaolima shamba namba 9, 10, 12, 13 na kuendelea wasipate huduma.
Previous
Next Post »