Dodoma. Mgogoro wa Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kuzuiwa kushiriki vikao vya Halmashauri ya Kilombero ambayo ina kata 10 za jimbo lake, umeingia bungeni baada ya kuitaka Serikali ieleze ni sababu ya kufanya ubaguzi.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Lijualikali alisema Jimbo la Kilombero lina halmashauri mbili; Ifakara na Kilombero na kwamba alizuiliwa kushiriki katika vikao vya Halmashauri ya Kilombero.
Alisema alipotaka kushiriki vikao hivyo alifungwa miezi sita, lakini mwenzake wa Ifakara ambaye ni wa CCM anaruhusiwa kushiriki vikao vya halmashauri zote.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene akijibu swali hilo alisema mbunge huyo ana halmashauri mbili.
“Kama zilivyo haki za wabunge wengine katika halmashauri zao, wanapaswa kuwa wajumbe wa vikao mbalimbali kama kamati ya mipango na fedha na Baraza la madiwani. Inakuwa vigumu kwa sababu mhusika alipaswa ku-balance interest za maeneo yote afanye ubunge wake.
“Lakini kinachotokea ni ambako mhusika pia ni diwani, diwani wa upande mmoja wa jimbo, kwa hiyo jambo hili haliwezi kufanana na la Bariadi na kwa sababu hiyo ana maelekezo yangu ambayo tulizungumza sana,” alisema.
Hata hivyo, Simbachawene alisema maelekezo hayo hayajatekelezwa na mbunge huyo na kumtaka aende ofisini ili walimalize jambo hilo.
Wakati huohuo, Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka alisema kauli ya Rais John Magufuli ya kuwa halmashauri itakayomuondoa au kumfukuza mkurugenzi itavunjwa, imeleta mkanganyiko nchini.
Hata hivyo, Simbachawene alikanusha kauli hiyo kuleta mkanganyiko na kwamba, imeainisha pale mkakati unapofanywa na madiwani kumuondoa mkurugenzi kwa masilahi binafsi.
Sign up here with your email