Mwanza. Baada ya mawakili wawili, Julius Mushobozi na Cosmas Tuthuru wanaowatetea mshtakiwa wanne na watano katika shauri la mauaji la aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow, kuweka pingamizi juzi la kutopokewa kwa hati ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wanne, Jaji Sirilius Matupa wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza alizikataa hoja hizo.
Hivyo, shahidi wa 17 upande wa Jamhuri, Salum Hamduni ambaye ni Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Dar es Salaam, aliendelea kutoa ushahidi wake na kueleza mahakama namna alivyowasafirisha watuhumiwa kutoka jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Precision hadi Mwanza.
Wakili Tuthuru aliweka pingamizi kwamba mshtakiwa hakupewa fursa ya kuulizwa kama anataka kuongeza au kurekebisha maelezo hayo, hali ambayo ni kinyume cha sheria na kumnyima haki yake. Hoja hiyo iliyoungwa mkono na Mushobozi.
Baada ya kuweka pingamizi hilo, wakili wa upande wa mashtaka, Robert Kidando alidai kuwa hoja hizo hazina msingi kwa sababu kwa mujibu wa shahidi, alisema alimuuliza mshtakiwa baada ya kuandika maelezo yake na kuyasoma mwenyewe na kumweleza kuwa ameelewa.
Wakili Kidando alidai hati hiyo inajieleza kuanzia mwanzo hadi mwisho wa maelezo, hivyo shahidi hakuwa na sababu ya kuendelea kumuuliza mambo mengine wakati mshtakiwa alisoma mwenyewe na kukubalina na maelezo hayo.
Jaji Matupa baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema Mahakama inayapokea maelezo hayo ya onyo kwa sababu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi hazitofautiani na zilizokuwa zimetolewa katika pingamizi la shahidi wa 16 na kuibua kesi ndogo.
Alisema kwa sababu maelezo ya onyo ya shahidi wa 16 aliyapokea, hivyo hata hayo hana sababu ya kutoyapokea kwani jambo ni lile lile.
Maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa sita, yaliwekewa pingamizi baada ya mshtakiwa kudai kuwa hayakuwa ya kwake, alilazimishwa kusaini na hakupewa fursa ya kuongeza au kurekebisha kitu chochote.
Katika uamuzi wa maelezo hayo yaliyosababisha kuibuka kesi ndogo, Jaji Matupa aliyapokea akisema baada ya kusikiliza pande zote mbili aliona hakuna nguvu iliyotumika kuandika maelezo hayo na kwamba, mshtakiwa alisomewa akakubaliana nayo.
“Hivyo, nayapokea ili kutoathiri mtiririko wa ushahidi,” alisema.
Hata hivyo, Wakili Mushobozi alieleza kwamba licha ya maelezo ya shahidi wa 16 yalipokewa, ilikuwa katika kesi ndogo na hii ni ya msingi hivyo kuna tofauti.
Hata hivyo, Jaji Matupa alisema ni kupoteza muda kurudia mambo ambayo amekwisha yatolea uamuzi na kusimamia uamuzi wake wa kuyapokea maelezo hayo, huku akisema atatoa sababu za kuyapokea kadri kesi inavyoendelea.
Baada ya mahakama kuyapokea maelezo hayo, Wakili Kidando aliendelea kumuuliza maswali shahidi huyo na katika maelezo yake, alidai alianza kuchukua maelezo hayo kwa mshtakiwa Oktoba 24, 2012 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 4:35 asubuhi katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Pia, alimuuliza kama angependa yatolewa mahakamani kama ushahidi, jambo ambalo shahidi huyo alikubaliana nalo.
Maelezo hayo yalionyesha mtiririko wa tukio lilivyokuwa kabla na baada kwa kuonyesha jinsi walivyoshirikiana kufanya uhalifu wa unyang’anyi, kwa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya majiji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Sehemu ya maelezo hayo, inasema mshtakiwa huyo wa tano, siku ya tukio la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow Oktoba 12, 2012 walikutana na wenzake eneo la Nyakabungo na kupanga maeneo ya kwenda kufanya uhalifu, wakiwa na bunduki aina ya shotgun.
“Tulivamia maduka, supermarket na grocery na kuiba simu, fedha na konyagi na katika maeneo ya Ghana walikuwapo wanywaji ambao niliwafunga miguu na wenzangu kuingia ndani na kupora, walipomaliza tukaondoka.
Baada ya kupora hapo, tulielekea Nyamanoro na penyewe tukapora, tulipotoka huko, wakati tulipofika maeneo Tai Five Kitangiri tukampora tena mwanamke simu saa 6:00 usiku.
Tulipomaliza tukavuka lami kupanda juu tukaona gari pikapu imepaki tukaikaribia, Muganyizi akasogea upande wa dereva, yule dereva alimuuliza nyie ni akina nani, wakajibizana na Muganyizi mimi nilisikia mlio wa bunduki ambayo alikuwa nayo Muganyizi.
Baadaye tuliona kuwa yule mzee alipigwa risasi, lakini tulimlalamikia kwa nini amemuua mzee huyo bila kuwa na hatia? Lakini baada ya kuona limeshatokea hilo tuliogopa na kila mmoja kusambaratika kivyake.
Mimi niliondoka Mwanza Oktoba 17, 2012 kuelekea jijini Dar es Salaam, kwa usafiri wa gari ya Kampuni ya Zuberi.
Baada ya tukio hilo, tulikutana tena Dar es Salaam eneo la Gongo la Mboto na kujipanga kuendeleza uhalifu mwingine.
Lakini Waikene alisema inabidi tutafute silaha nyingine kwa sababu Jiji la Dar es Salaam ni kubwa, hivyo hatuwezi kufanikiwa tukiwa na kasilaha kamoja huku akisema kuna sehemu anafahamu ambako kuna mlinzi analinda na silaha hivyo tukampore.
Tulifanya hivyo kwa kuvamia kampuni moja na kumnyang’anya mlinzi silaha, katika tukio hilo Muganyizi alipigwa na kitu kichwani na kuumizwa wakati wa purukushani wa kutaka kunyang’aya silaha hiyo.
Hata tulipokamatwa gesti tulikuwa tunatoka kufanya uvamizi na kupora maeneo mbalimbali.
Kwenye begi tuliyokuwa nayo wakati tunakamatwa, kuna waya mwekundu uliokuwamo na bunduki, ule waya unatumika kutoa risasi kama imeg’ang’ania kwenye magazini.”
Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, Wakili Kidando aliendelea kumuuliza shahidi huyo kilichoendela baada ya kuandika maelezo ya onyo.
Wakili: Baada ya kumaliza kuandika maelezo yake ulifanya nini tena?
Shahidi: Nilimuuliza mshtakiwa kama ameelewa.
Wakili: Alijibu nini baada ya kumuuliza hivyo?
Shahidi: Alisema ameelewa na alisoma mwenyewe akasaini na mimi nikasaini, kisha nikayapeleka kwa bosi wangu.
Wakili: Baada ya kuwa umemaliza kufanya hayo yote, kuna kitu gani kingine kiliendelea?
Shahidi: Nakumbuka Oktoba 29, 2012, nilipewa jukumu la kuwasafirisha watuhumiwa kutoka Dar es Salaam kuwaleta Mwanza kwa ajili ya taratibu zingine.
Wakili: Ulisafirisha watuhumiwa wangapi na kwa usafiri gani?
Shahidi: Nilisafirisha watuhumiwa watano kwa ndege ya Shirika la Precision.
Wakili: Unawakumbuka hao uliowasafairisha?
Shahidi: Ndiyo nawakumbuka, alikuwa Muganyizi Peter (mshtakiwa wa kwanza), Chacha Waikene (mshtakiwa wa pili), Magige Marwa (mshtakiwa tatu), Bhoke Marwa (mshtakiwa wanne) na Buganzi Edward (mshtakiwa wa tano).
Wakili: Baada ya kufika Mwanza nini kiliendelea?
Shahidi: Walikabidhiwa kwa afande Konyo, kisha shughuli za upelelzi zikaendelea.
Baada ya wakili wa Serikali kumaliza kumuongoza shahidi huyo, Wakili James Njelwa anayemtetea mshtakiwa wa kwanza aliiomba mahakama iaharishe shauri hilo kwa madai mawakili wote saba wa upande wa utetezi, hawataweza kumuuliza maswali shahidi wakamaliza kulingana na muda uliokuwa umebaki.
Pia, alidai Wakili Ngasa Maduhu anayemteta mshtakiwa wa sita anaumwa anatakiwa kwenda hospitali, Jaji Matupa alikubaliana na hoja hizo na kuahirisha shauri hilo hadi kesho mawakili hao watakapoanza kumuuliza maswali shahidi huyo.
Sign up here with your email