Mmmh! Sakata ya kuwakata wote hao wenye cheti feki imechokoza mijadala mingi. Kama kawaida, wengine wamenitumia mabomu yao. Hebu tuwasikilize kidogo.
Makengeza,
Kumbe mkuki kwa nguruwe, haumgusi binadamu. Duh! Upande mmoja wako karibu 10, 000 ambao wametambuliwa na kutumbuliwa bila huruma. Sasa wengine wanaonekana wametumikia taifa kwa udi na ubani miaka nenda rudi. Ndiyo maana, inabidi kuelewa kwamba hawajatumbuliwa kwa kukosa stadi na maarifa au hata ari ya kazi na uzalendo. Walikuwa hawapimwi kwa mambo hayo. Wametumbuliwa kwa sababu walighushi kama ambavyo mwizi anashtakiwa kwa wizi hata kama ametumia vizuri fedha zake za wizi kwa maendeleo ya Taifa.
Ndiyo maana suala la kwamba wanasiasa wanahitaji kujua kusoma na kuandika si hoja pia. Nilirudi kuangalia maana ya kusoma na kuandika ni nini. Darasa la pili si wanaweza kusoma:
Juma ni mvulana. Juma anapenda mpira. Juma anacheza mpira kila Jumamosi.
Maswali
Juma ni nani?
Juma anapenda nini?
Juma anafanya nini kila Jumamosi?
Hili ni zoezi zuri sana na nadhani tunaweza kutunga mtihani maalumu kwa hawa waheshimiwa wa kuchaguliwa na kuteuliwa pia ili, kabla ya kuapishwa kwa wanaotakiwa kujua kusoma na kuandika tu, itabidi wafanye kamtihani maalumu wa kusoma kwa sauti na kujibu maswali. Nimejaribu kutunga mwenyewe:
Mimi ni mbunge.
Napenda sana kuwa mbunge.
Baada ya kuwa mbunge sina haja ya kusoma tena.
Nakaa kwenye viti vizuri.
Nawasikiliza wengine.
Nasikiliza hoja zao.
Kisha naweza kusema na mimi.
Kusema bila kusoma ni raha sana.
Kuwa mbunge ni raha sana.
Maswali
1. Nani anapenda kuwa mbunge?
2. Anakaa wapi?
3. Wakati gani anasema?
4. Kwa nini kuwa mbunge ni raha sana.
Waheshimiwa wanisamehe lakini maana niliona nikiongeza neno ‘mheshimiwa’ ili lisomwe, linaweza kuwatatiza wengine.
Na kwa wakuu wengine, tunaweza kutengeneza vimatini kama hivi ili wasome kabla ya kuapishwa. Hapo tutaridhika kwamba vigezo muhimu wamevizingatia.
Lakini kama nilivyosema, suala si wingi wa kisomo, suala ni uhalali wa kisomo. Wengine waliofukuzwa juzi ni wataalamu wa hali ya juu, lakini walighushi, basi. Kughushi ni kughushi kwa hiyo hata hawa wenye kujua kusoma na kuandika, haijalishi ni wachapakazi namna gani, haitoshi kama wanaweza kusoma kwa kirusi na kichina pia. Kughushi ni kughushi tu. Vyote sawa, vyeti sawa.
Mwingine hakukubali.
Makengeza,
Kwanza ni muhimu kukagua vyeti vya kila mtu. Sekta ya umma, sekta binafsi, wateuliwa na waajiriwa, sekta rasmi na isiyo rasmi. Tuwajue wote waliokosa. lakini dawa ya kukosa ni moja tu? Ni lazima wafukuzwe tu? Mbona wahalifu wengine wanapigishwa faini tu? Hata wezi. Hivyo, kwa nini wasisimamishe kazi badala ya kufukuzwa, walipishwe faini kwa sababu ya kughushi, kisha wapewe nafasi ya kuthibitisha uwezo wao baada ya miezi kadhaa?
Ndiyo! Sote twajua kwamba kuna shule nyingi ambazo ni feki pia, hata zamani. Sisi tuliosahihisha mitihani ya taifa toka miaka ya 1980 tulijua kuna shule nyingi ambazo husahihishi mwanafunzi, unasahihisha shule maana ilikuwa ni dhahiri kwamba hawakufundishwa kitu.
Sasa mwanafunzi wa shule hizo, hata akiwa na akili ya Einstein, bado atafeli maana hajafundishwa kitu. Hapo akitaka maendeleo, anaenda mahali pengine na kughushi ili aweze kusonga mbele.
Na kweli hapo mbele anakuta asasi nzuri ya elimu na kufanikiwa na baada ya hapa ameweza kutumikia taifa vizuri. Sasa kweli amekosea lakini asasi za elimu na mfumo mzima umemkosesha pia. Apewe adhabu ndiyo lakini baada ya hapo apewe nafasi ya kuthibitisha uwezo wake tusipoteze utaalamu na uzoefu wake.
Mwingine alienda mbali zaidi.
Makengeza, mbona tunaongelea vyeti feki, vyeti feki vya mtu mmojammoja tu. Wao walipitia kwenye asasi gani za elimu? Hizi asasi zote kweli zilitoa elimu au zilibatizwa na jina la shule tu na kuachwa.
Nakuambia. Ukitaka kuanzisha shule ya walio na ukata, utapewa masharti kibao. Wenye uwezo lazima wahakikishe kwamba shule wanaposoma watoto wao zinafikia viwango vya hali ya juu. Lakini shule za ukata wapi na wapi? Najua Wizara ya Mashule (maana sijui kama kweli ni Wizara ya Elimu) ina viwango vya lazima kwa kila shule, yaani idadi ya walimu, idadi ya madarasa na vyoo na kadhalika, idadi ya wanafunzi kwa kila mwalimu.
Wanatumia viwango hivi kwa ajili ya shule za wengine lakini si kwa ajili ya shule zao, kwa nini? Kwa nini wasianzishe msako wa shule feki. Ndiyo, wazazi wataumia najua lakini wataumia kwa sababu tayari wanadanganywa na hawajui.
Wanahangaika kumpeleka mtoto wao shule wakitegemea atapata maisha bora zaidi kutokana na kuelimika. Kumbe kwenye shule nyingi hizi elimu ni adimu au haipo. Bora mtoto akae nyumbani na kutafuta njia nyingine ya kuelimika kuliko kukaa kila siku bila mwalimu, bila kitabu.
Tena sijui hawa watu wa wizara ya mashule wana u-mbuni wa namna gani. Zifanyike tafiti ngapi za kuonyesha kwamba katika shule nyingi, wanafunzi wanafundishwa saa moja au mbili kwa siku? Walimu hawapo au walimu hawataki kuwepo. Kisha tunageuka na kuwalaumu vijana kwa kuharibika. Unategemea nini katika hali hii?
Kwa hiyo, hebu tupitishe msako wa shule feki nao zifungwe hadi zinafikia viwango vinavyotakiwa. Bora shule chache zinazofundisha kuliko magodauni mengi ya kurundika vijana tangu asubuhi hadi mchana hadi waoze.
Na usiseme kwamba mimi ni mbaguzi eti mbona watoto wa wenyewe wanasoma sasa unataka kufunga shule zetu za sisi wenye ukata ili watoto wetu wasipate elimu. Wanapata elimu wakiwa ndani ya shule hizi? Hata ukiangalia matokeo ya baraza la mitihani. Kwelikweli vijana wote wa shule fulani wakipata sufuri au sufuria tupu au divisheni kumi unaweza kusema hii ni shule? Baada ya miaka minne, hakuna hata mmoja anayejua kitu. Haiyumkiniki. Tunadanganyana kweli aisee.
Sign up here with your email