CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kinatowa pole kwa wananchi wote walioathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote.
Mvua hizi zinazoendelea kunyesha zimeathiri maeneo mbali mbali hasa katika kisiwa cha Pemba. Maeneo hasa yalioathiriwa yakiwemo Vijiji vya Mbuyuni, Mwambe, Uweleni, Makombeni, Ukutini, Kendwa, Vitongoji, Chamanangwe na maeneo mengine katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba. Pia zimeathiri miundombinu, majengo ya wananchi na ya Serikali.
Pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuendelea kufanya tathmini ya kitaalam juu ya kubaini athari kubwa zinazotokana na mvua hiyo. Chama cha Mapinduzi Zanzibar kinaishauri Serikali na Asasi nyengine kwa msisitizo mkubwa zichukue hatua za haraka za kupeleka misaada ya dharura kwa Wananchi wa maeneo yaliyopata na athari za mvua hiyo ili kunusuru kutokea kwa majanga mengine yakiwemo njaa, maradhi ya miripuko n.k.
CCM inawaomba wananchi wa Kisiwa cha Pemba na maeneo mengine kuendelea kuwa na subira, utulivu katika kipindi hichi kigumu, huku Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali zikiendelea kushughulika na kutafuta ufumbuzi wa haraka juu ya kutatua matatizo hayo ili wananchi warejee katika hali zao za kawaida.
Aidha Chama cha Mapinduzi kinawasihi Wahisani, Marafiki wa ndani na nje ya Nchi, watu wenye uwezo popote walipo kujitokeza kuchangia misaada ya Kibinadamu katika athari hizi za mvua zilizojitokeza.
Mwisho, tunawaomba wananchi wa maeneo mbali mbali hasa wale wanaoishi katika maeneo ya hatarishi kuchukua tahadhari, sambamba na kufuata kanuni za kiafya ili kuepukana na majanga mengine.
Sign up here with your email