POINT ZA MSIMBAZI ZARUDISHWA MEZANI - Rhevan Media

POINT ZA MSIMBAZI ZARUDISHWA MEZANI



Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umeitisha kikao cha Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za wachezaji kujadili barua iliyowasilishwa na uongozi wa Kagera Sugar kuomba marejeo ya mchezo wa Kagera Sugar na Simba uliochezwa April 2, katika Mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ina mamlaka ya kutafsiri Sheria na Kanuni za soka nchini kama ilivyoainishwa kwenye Katiba na sehemu ya utangulizi ya kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema sababu ya kuitisha kikao hicho ni kutokana na barua ya Kagera Sugar inayotaka kupitiwa upya kwa hukumu iliyotolewa na Kamati ya Saa 72.
“Kamati hii kazi yake ni kutafsiri Sheria, Kanuni na Katiba ya TFF na ndio maana Kagera wamepeleka shauri lao, tunaamini pande zote zinazohitajika zitafika kwenye kamati na kutoa ushirikiano. TFF inasisitiza wanafamilia wa mpira kuzisoma Kanuni na Sheria zinazoongoza soka letu,” alisema Lucas.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Aprili 2 na kumalizika kwa Kagera kuifunga Simba mabao 2-1, Simba ilikata rufani ikidai beki wa Kagera, Mohammed Fakhi alicheza mechi hiyo akiwa na kadi tatu za njano.
Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Saa 72 ilikutana Alhamisi iliyopita na kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa Fakhi alicheza akiwa na kadi tatu za njano.
Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa soka na kocha wa zamani wa Tanzania Prisons na Ashanti, Joseph Kanakamfumu alisema hakukuwa na ulazima wa kuwaita waamuzi wa mechi ya Kagera na African Lyon.
“Mchezo huo ulichezezwa na waamuzi wanne, kwanini kamati iite waamuzi wakati tayari walitoa ripoti. Huku ni kuendelea kuwachanganya watu na kulifanya suala hili kuwa gumu.
“Sasa wanalazimika kuwaita Kagera na watalazimika kuwaita hata African Lyon,” alieleza Kanakamfumu.
Kocha huyo alisema mzozo kuhusu suala hilo, unapunguza ladha kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kuona zinaonewa na nyingine zikipendelewa.
Simba sasa imefikisha pointi 62 baada ya sare yao ya jana dhidi ya Toto African, ikiizidi Yanga pointi sita. Hata hivyo, Yanga ambayo jana ilikuwa ikirudiana na MC Alger kuwania kucheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ina mechi mbili mkononi.
Previous
Next Post »