Ndanda inataka pointi sita za Kanda ya Ziwa ili ziwaweke salama kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuangalia mipango mingine.
Ndanda ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 30 na ipo katika hatari ya kushuka daraja pamoja na timu sita zilizo chini yake na tatu zilizo juu kwenye msimamo wa ligi.
Timu hiyo iliweka kambi ya wiki moja mkoani Singida kuiwinda Mwadui inayopambana nayo leo kusaka pointi muhimu zitakazozidi kuwaweka salama kwenye msimamo wa ligi.
Kocha wa kikosi hicho, Meja mstaafu, Abdul Mingange alisema wanataka pointi sita Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui kesho na Stand United Alhamisi ili kuwaweka salama zaidi kwenye msimamo wa ligi.
Meja Mingange alisema kama watapata pointi hizo watatakiwa kushinda mechi moja kati ya mbili watakazobakiza ili kujinusuru na panga la kushuka daraja.
“Ligi imekuwa ngumu kwa sababu ukiangalia tunapishana pointi chache na washindani wetu na kila mtu hataki kushuka, hivyo kazi ni nzito.
“Tumejipanga kupata pointi sita huku Kanda ya Ziwa ninajua haitakuwa kazi rahisi, lakini nimewaambia wachezaji wangu ni jinsi gani ilivyo muhimu kushinda michezo hiyo miwili kama tunataka kubaki salama kwenye ligi,” alisema Meja Mingange.
Alisema hawaangalia wapinzani wao wanafanya nini ingawa wanawaombea mabaya ili iwe kazi rahisi kwao kubaki kwenye ligi msimu ujao.
Sign up here with your email