WAFANYABIASHARA WA ASALI WAPEWA MASHARTI - Rhevan Media

WAFANYABIASHARA WA ASALI WAPEWA MASHARTI

Tokeo la picha la asali mbichi

WAFANYABIASHARA wa asali wilayani Ikungi mkoani Singida, wanaoendesha shughuli zao kando mwa barabara kuu ya Singida-Dodoma, wamepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia sasa kutumia vifungashio halisi badala ya chupa za konyagi ili kulinda afya za walaji.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa matumizi sahihi ya vifungashio vya asali iliyofanyika katika Kijiji cha Issuna wilayani humo.
Alisema ufungashaji wa asali unaofanywa na wafanyabiashara wa asali katika Wilaya ya Ikaungi, si wa kuridhisha na kwa namna moja au nyingine unachangia kuharibika kwa asali.
“Ufungashaji unaofanywa na wafugaji wetu wa nyuki unachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa soko la asali. Wafanyabiashara hawa wanaouza asali pembezoni mwa barabara wanafungasha asali bila kuzingatia sheria na kanuni za biashara ya mazao ya nyuki hususani asali. Nawapeni mwezi moja mbadilike katika ufungashaji,” alisisitiza Mtaturu.
 Mkuu wa wilaya hiyo amewataka wafanyabishara hao wa asali kufanya shughuli zao ndani ya jengo maalumu la kuuzia mazao ya nyuki ambalo tangu lilipomalizika kujengwa mwaka 2013 hadi sasa halijawahi kutumiwa.
Awali Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Ikungi, Samson Lyimo, alisema asilimia 70 ya eneo la ardhi ya Wilaya ya Ikungi ni misitu, miti, vichaka na nyanda za nyasi au mbuga ambayo ni rasilimali muhimu kwa ufugaji wa nyuki.
“Ufugaji wa nyuki Wilaya ya Ikungi unafanywa na mtu mmoja mmoja na wengine wamejiunga katika vikundi na kufanya shughuli kwa pamoja. Hadi sasa tunavyo vikundi 63 ambavyo vimesajili na vinajihusisha na uzalishaji wa mazao ya nyuki ambayo ni asali na anta,” alisema Lyimo.

Previous
Next Post »