SHEREHE ZA WIKI YA MAJI KUWA KAVUKAVU - Rhevan Media

SHEREHE ZA WIKI YA MAJI KUWA KAVUKAVU

Tokeo la picha la WIKI YA MAJI

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amesema maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka huu hayatakuwa na sherehe kama ilivyo kuwa miaka ya nyuma.
Amesema badala yake maadhimisho yake, yatahusisha shughuli za uwekaji mawe ya msingi na kutembelea vyanzo vya maji.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji, ambayo kilele chake kinatarajiwa kuwa Machi 22, mwaka huu, Lwenge alisema miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu wa wizara hiyo, kuendesha shuguli za maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa kufanya sherehe na maonesho katika maeneo mbalimbali nchini.
“Katika maadhimisho ya mwaka huu kutakuwa hakuna sherehe zozote shughuli zitakazofanyika ni kuweka mawe ya msingi, kutembelea miradi mipya pamoja na vyanzo vilivyo kauka ambavyo vilikua vinatumika awali,” alieleza.
Aliongeza kuwa maadhimisho hayo, yatawalenga wananchi kwa kutembelea katika maeneo yao na kujionea vyanzo vya maji vilivyopo na vile vilivyo kauka ili kuweza kuwapa elimu ya kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu.
“Leo hii kama utamchukua mwanachi na kumpeleka katika chanzo ambacho kimekauka akajionea akitoka pale atakuwa amepata somo kubwa sana hilo ndilo tunalotaka lifanyike,” alifafanua na kuongeza kuwa katika Wiki ya Maji, watahamasisha wananchi kupanda miti pamoja na kuvuna maji ya mvua pamoja na kujenga mabwawa.
Alisema kama serikali tayari wana mpango wa kujenga mabwawa, ambayo yatatumika kuvuna maji, lakini pia wanachi watapewa elimu kupitia maadhimisho hayo namna ya kujenga mabwawa, ambayo yatawasaidia kuvuna maji kwajili ya kilimo cha umwagiliaji na shughuli nyingine za kiuchumi.
Alisema lengo la serikali ni kuwafikishia Watanzania huduma bora ya majisafi na uondoaji wa majitaka kwa wananchi wengi waishio mijini na vijijini.
Alisema sasa wastani wa upatikanaji wa maji nchini ni asilimia 72.15 kwa wakazi wa vijijini, asilimia 86 kwa wakazi wa mjini na asilimia 75 kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Pia alisema malengo ya kitaifa ni kufikia asilimia 85 kwa wakazi wa vijiji na asilimia 95 kwa wakazi wa mijini ifikapo mwaka 2020, katika kukamilisha malengo hayo serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ambayo inatoa mchango katika kupunguza umaskini.
Previous
Next Post »