SERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUFUNGA NDOA BILA CHETI CHA KUZALIWA - Rhevan Media

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUFUNGA NDOA BILA CHETI CHA KUZALIWA

1 unnamed
Serikali  imepiga marufuku watu kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hayo leo akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kuongeza kuwa serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia wageni kuingia kinyemela nchini.
Pamoja na mambo mengine, Dk.Mwakyembe amewataka Wakala wa Usajili wa vizazi na Vifo (RITA), kuhakikisha inasimamia sheria ya usajili ambapo amesema kuwa bila kuwa na  takwimu sahihi  za  vizazi na vifo ama ndoa  inasababisha nchi kushindwa kusonga mbele kimaendeleo.
“Wenzetu nchi zilizoendelea suala la usajili wamelipa kipaumbele lakini sisi bado tuko nyuma, kwa mfano Mkoa wa Morogoro  kwa mujibu wa sensa  ya watu na makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuna jumla ya wakazi milioni 2.2, lakini waliosajiliwa na kuwa na vyeti  vya kuzaliwa ni asilimia 11 pekee huku wengine wakiwa bado hawasajiliwa,” amesema.
Dk. Mwakyembe pia ametumia nafasi hiyo kuwaonya watendaji wa mahakama watakaolalamikiwa na wananchi kufanya kazi kinyume na maadili ikiwamo upokeaji wa rushwa ama kutotenda haki na kutumia  mahakama kugeuza kesi za madai kuwa kesi za jinai.
Previous
Next Post »