POLISI visiwani Zanzibar imewakamata wanaume 16 wanaodaiwa kufanya mapenzi ya jinsia moja, katika operesheni maalum inayoendelea kwenye mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa mkoa huo, Ayoub Mohammed, alisema mashoga hao waliokamatwa walipelekwa hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na kubaini iwapo wanafanyiwa vitendo hivyo.
Alisema kati yao 11 walibainika wanajihusisha na mapenzi ya jinsi moja na tayari majalada yao yameshafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kwa ajili ya kushitakiwa.
Alisema kuwa watuhumiwa wengine wanaendelea kuchunguzwa na uchunguzi utakapokamilika majalada yao ripoti itaamua hatua za kuwachukulia iwapo wanapelekwa kwa DPP au wanaachiwa.
“Kazi ya kuwasaka mashoga inaendelea na tutahakikisha tunawakamata ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo havikubaliki kisheria, kimaadili wala kijamii,”alisema.
Aidha, alisema operesheni hiyo itawahusu pia wale wanaojifanya waume na kuwafanyia vitendo hivyo wenzao ili wakamatwe.
Aliwataka mashoga kuwataja wale wote wanaowafanyia vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwani ushoga umekuwa ukiidhalilisha jamii.
“Idadi ya matukio ya udhalilishaji hasa kwa watoto yamekuwa yakiongezeka na hivi sasa vitendo hivyo vimeshamiri kwa watoto wa kiume kulawitiwa,” alionya.
Aliitaka jamii kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhudi hizo za kuwasaka na kuwakamata wanaojihusisha na vitendo hivyo ili kuinusuru Zanzibar na wimbi la udhalilishaji na maradhi.
Alisema kitendo hicho kimekuwa kikipoteza nguvu kazi ya taifa kutokana na vijana wengi wa kiume kujihusisha na vitendo hivyo ambayo athari zake ni magonjwa na vifo.
“Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa hili tukisema vitendo hivi tunavifumbia macho tutakosa nguvu kazi ya taifa,”alisema.
Sign up here with your email