TAARIFA za upelelezi wa kesi ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo inayomkabili mfanyabiashara, Yusuf Yusuf, maarufu Mpemba na wenzake sita, bado ina utata.
Kutokana na hali hiyo, mahakama imeiamuru Jamhuri, kuwasilisha taarifa kamili Machi 20, mwaka huu.
Amri hiyo ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya Mwendesha Mashitaka, Inspekta Hamis Said, kudai upelelezi haujakamika.
“Hapa siyo mahali pa kudampu washtakiwa, mwendesha mashtaka waeleze tunachukia hali hii na tunategemea kupata taarifa sahihi na kama RCO anatukwamisha, tutamuita kwa jina lake,”alisema Hakimu Simba.
Wakati Hakimu Simba akisema hayo, Wakili wa Utetezi, Aloyce Komba, aliomba upande huo ueleze hatua za kesi hiyo ilipofikia baada ya kila siku kueleza taarifa za jalada, kwamba liko kwa RCO (mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai), Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Alidai washtakiwa wapo mahabusu tangu Novemba, mwaka jana kesi ilipotajwa na wahusika walijua upelelezi umekamilika.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 20, mwaka huu na kuutaka upande wa Jamhuri siku hiyo ueleze taarifa kamili ya maendeleo ya shauri hilo.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, dereva Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.
Sign up here with your email