KASI YA MAPAMBANO ZIDI YA DAWA ZA KULEVYA YAINGIA ZANZIBAR - Rhevan Media

KASI YA MAPAMBANO ZIDI YA DAWA ZA KULEVYA YAINGIA ZANZIBAR



Dar es Salaam. Wakati mapambano dhidi ya watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya yakiendelea kushika kasi hapa Bara, safari hii vita hivyo vimeingie visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ameagiza kupanguliwa kwa maofisa wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wa Idara ya Polisi na Uhamiaji waliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume mjini Unguja.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mara baada ya Masauni kutembelea uwanja huo na Bandari kuu ya Zanzibar, ilisema kuwa baadhi ya maofisa wamekuwa na tabia ya kuzima mashine za ukaguzi wa mizigo kwa makusudi ili kupitisha vitu haramu zikiwamo dawa za kulevya.
“Ingawa polisi wana kitengo maalumu cha kupambana na dawa hizi, lakini bado tatizo hili linazidi kushamiri hapa Zanzibar,” alisema Mhandisi Masauni katika taarifa hiyo.
Pia, naibu waziri huyo ameagiza wafanyakazi wa idara ya uhamiaji na polisi waliofanya kazi katika eneo moja kwa zaidi ya miaka miwili kuhamishiwa kwenye vituo vingine ili kusaidia kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya visiwani humo.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Masauni aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Ahmada Salum.
Mkuu wa idara ya uhamiaji uwanjani hapo, Kamishna Msaidizi Fulgence Mutarasha alisema katika vita ya kupambana na dawa hizo mwaka jana waliwakamata abiria 29 na kuwaweka chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi. 







ADVERTISEMEN
Previous
Next Post »